Tunachokifahamu kuhusu 'utata' wa mazungumzo ya Marekani na Iran

d

Chanzo cha picha, Getty Images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Utata kuhusu mazungumzo ya kumaliza vita ya Israel, Marekani dhidi ya Iran, umeibuka hivi karibuni, ukichochewa na kauli za Rais wa Marekani, Donald Trump, na kukanushwa kwa pande za Iran.

Kauli za pande zote mbili zinapingana, huku Trump akisisitiza kwamba mazungumzo "yanaendelea" kati ya Marekani na Iran na kwmaba Iran inaonyesha utayari mkubwa wa kufikia makubaliano, lakini viongozi wa Tehran wakiuka madai hayo na kuyaita "habari za uongo".

Hali hii ya kupinga inaashiria hali ngumu katika diplomasia ya Mashariki ya Kati. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mashambulizi ya kijeshi yamekuwa yakiendela kama kawaida kati ya Iran na Israel, huku Marekani ikiendelea kuonyesha uwepo wake wa kijeshi katika eneo hilo.

Hata hivyo, juhudi za kidiplomasia za kuanzisha mazungumzo haya zimeripotiwa kuanza kitambo, hata kabla ya mlipuko wa mashambulizi ya kijeshi yaliyoanza mwezi uliopita. Lakini utata wa sasa unaongeza joto.

Nani anasema nini kuhusu mazungumzo?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Trump

Rais Donald Trump amekuwa mstari wa mbele kutoa taarifa kuhusu mazungumzo. Ameeleza kwamba Marekani inazungumza na "watu sahihi" ndani ya Iran na kwamba viongozi wa Iran wanataka "kufanya makubaliano kwa nguvu zote."

Amesema kwamba mazungumzo haya yanashughulikiwa na maafisa wake wakuu, wakiwemo Makamu wa Rais JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio.

Trump pia amesisitiza kuwa utawala wake umepewa kile alichokitaja kama "zawadi kubwa" kutoka kwa Iran, kinachohusiana na masuala ya mafuta na usalama wa mkondo wa bahari wa Hormuz.

Hata hivyo, upande wa Iran umekanusha taarifa hizi. Viongozi wakuu, akiwemo Spika wa Bunge Mohammad-Bagher Ghalibaf, wamesema kwamba hakuna mazungumzo rasmi yaliyofanyika na Marekani.

Iran inatambua tu baadhi ya masuala yaliyotolewa kupitia wapatanishi, na hiyo haimaanishi mazungumzo rasmi yenye mabadiliko yoyote yameanza. Utata unaongeza, huyu anayaona ni mazungumzo, huyu anaona vingine.

2. Mambo 15 ya Marekani mezani kwa Iran

Ingawa hakuna orodha rasmi iliyotolewa, vyanzo vya kidiplomasia vinaonyesha kwamba masuala takribani 15 yamewasilishwa na Marekani kwenye meza hiyo ya mazungumzo. Yanatajwa kuhusisha pia masuala ya nyuklia, usalama wa mafuta, na uwepo wa kijeshi.

Sharti la kudhibiti mpango wa nyuklia wa Iran linaonekana kuwa jambo kubwa na muhimu ambalo Marekani linatilia mkazo. Trump ameandika kwamba Iran imekubali kutokuwa na silaha za nyuklia, madai ambayo Tehran haijathibitisha rasmi. Utata mwingine.

Suala lingine ni usalama wa mkondo bahari wa Hormuz, ambapo Trump amesisitiza kwamba zawadi iliyotolewa na Iran ni ya kipekee katika masuala ya mafuta na gesi, na kuimarisha msukumo wa Marekani katika eneo hilo.

Wachambuzi wanasema pia kwamba baadhi ya hoja zinazojadiliwa zinaweza kujumuisha uwekaji wa mipaka ya kijeshi na kupunguza uwepo wa vikosi katika eneo hilo, ingawa haya bado hayajathibitishwa rasmi.

3. Pakistan na nchi za tatu kama wapatanishi

Pakistan imeonekana kuwa miongoni mwa nchi zinazochukua nafasi ya upatanishi. Kupitia njia zisizo rasmi, Pakistan inaripotiwa kuwa na jukumu la kuwasilisha ujumbe kutoka pande zote mbili.

Nchi nyingine Uturuki na Misri, pia zinaweza kushirikiana katika njia hizi za kidiplomasia ili kuhakikisha usalama na utulivu wa mazungumzo bila kuibua mkazo mbele ya umma. Zinatajwa kuwa sehemu ya mpango wa muda mrefu wa kuleta amani eneo hilo la Mashariki ya Kati.

Hata hivyo, njia hizi za kidiplomasia zisizo rasmi hazijafunguka kwa umma na bado hazina uthibitisho wa pande zote.

Hatua hii ni ya msingi kuelekea makubaliano yoyote ya amani. Amani ambayo wananachi hasa wa Iran wanayatamani baada ya kueleza hisia zao kwamba wanatamani mazungumzo yafanyike na vita vimalizike. Lakini bado kuna maswali mengi yanayobaki bila majibu.

4. Maswali makubwa?

s

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mazungumzo yanadaiwa kuendelea na vita vinaendelea
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hadi sasa, hoja kadhaa bado hazijajibiwa: Je, mkataba wowote utahusisha kudhibiti mpango wa nyuklia wa Iran? Je, zawadi iliyotajwa na Trump inahusisha nini hasa, na je itakuwa na athari gani katika eneo la mashariki ya kati?

Maswali mengine yanayosalia ni Je, njia za kidiplomasia zisizo rasmi zitafanikiwa kuleta mabadiliko halisi? Na hatimaye, je, makubaliano yoyote yataleta mwisho wa vita vinavyendelea Mashariki ya Kati?

Lakini maswali yenye utata ni utata wa suala lenyewe la mazungumzo, kwanini Iran inakataa kwamba hakuna mazungumzo yanayoendelea, huku Trump akisema mazungumzo yanaendelea na Iran inayataka mazungumzo hayo kwa udi na uvumba. Nani anadanganya na kwa nini?

Mmoja wa wachambuzi wa masuala ya usalama anasema, utata huu ni masuala ya kawaida hasa nchi zinapokuwa vitani, kuna wakati taarifa zinafichwa ama zinatolewa kwa maslahi ya kivita.

Hadi sasa, hakuna uthibitisho wa mazungumzo rasmi yaliyoimarisha amani, na hali ya kisiasa na kijeshi inabaki kuwa yenye wasiwasi mkubwa, kwa sababu mashambulizi ndiyo kwanza yanaongezeka kati ya pande zinazopigana.