Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mji wa Iran 'washambuliwa vibaya', huku video ikionyesha milipuko mikubwa kwenye kituo cha makombora
Picha kutoka mji wa Isfahan nchini Iran, iliyothibitishwa na BBC, inaonyesha milipuko mikubwa kwenye kambi hiyo - inaonekana baada ya shambulizi la anga ama la Marekani au Israel.
Muhtasari
- Milipuko mikubwa yaripotiwa katika kituo cha makombora Iran
- Katibu Mkuu wa UN atoa wito kwa Marekani na Israel kusitisha vita
- Iran yatoa onyo kali, Trump atishia mashambulizi makubwa zaidi
- Watoto wanne wauawa kwa shambulio la kisu Uganda
- Mlango Bahari wa Hormuz uko wazi kwa meli ambazo si za "adui"
- Raia 1800 wameuawa tangu utawala wa kijeshi kuchukua madaraka Burkina Faso- Ripoti
- Marekani imemuondelea vikwazo rais wa mpito wa Venezuela Delcy Rodriguez
- Trump aziambia nchi zinazotegemea mafuta kutoka Ghuba kuingilia kati mkwamo wa Hormuz
- Sekta ya majani chai nchini Kenya yaathirika na vita vya Iran
- Kiongozi wa kijeshi Libya anunua ndege zisizo na rubani licha ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa
- Milipuko katika ghala la risasi yawaua watu 13 Burundi - jeshi
- Vita vya Iran: Hotuba ya Trump yatikisa masoko huku bei ya mafuta ikipanda
- Tetemeko la ardhi la ukubwa wa 7.4 lakumba Indonesia
- UAE inazuia makombora yaliyorushwa na Iran
- Tazama wakati Artemis iIiporuka angani kwenye safari ya kihistoria
- Vita vya Iran: Trump asema malengo ya Marekani 'yanakaribia kukamilika'
Moja kwa moja
Na Ambia Hirsi, Asha Juma, Beldeen Waliaula & Martha Saranga
Milipuko mikubwa yaripotiwa katika kituo cha makombora Iran
Video zinazoonyesha milipuko mikubwa karibu na kituo kikubwa cha makombora nchini Iran nje kidogo ya eneo la Isfahan zimethibitishwa.
BBC Verify imechunguza video tatu zilizosambazwa kwa mara ya kwanza kwenye mitandao ya kijamii hapo jana, ikiwemo moja inachoonyesha moshi mwingi na uchafu wa moto hewani karibu na kituo cha makombora cha Isfahan Kusini.
Mwanamume aliyerekodi anaelezea alivyoshtushwa na mlipuko huo.
Video inaonyesha moto katika uwanja wa ndege wa Iran kufuatia mashambulizi yaliyoripotiwa
BBC Verify imechunguza video ya moshi mkubwa ukipanda karibu na uwanja wa ndege mkuu huko Mashhad, mji ulio kaskazini mashariki mwa Iran.
Video iliyothibitishwa ilionyeshwa kwa mara ya kwanza asubuhi ya leo na ilirekodiwa kwenye gari lililokuwa likiendeshwa karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mashhad.
Tuliweza kuthibitisha kuwa ilikuwa ikisogea kando ya barabara kuu karibu na Mashhad kwa kutambua alama muhimu na kuzilinganisha na picha za mwonekano wa barabara.
Ripoti za vyombo vya habari vya Iran zinasema hifadhi kubwa za mafuta na maghala huenda yalilengwa. Uwanja wa ndege pia una mojawapo ya vituo vya anga vya jeshi la anga la Iran, lakini haiwezekani kutambua kilichochambuliwa kutoka kwenye video hiyo.
Soma zaidi:
Katibu Mkuu wa UN atoa wito kwa Marekani na Israel kusitisha vita
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amezungumza na waandishi wa habari mjini New York, ambapo ametoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa vita na uhasama kutoka pande zote.
"Tuko karibu na vita vikubwa ambavyo vitaikumba Mashariki ya Kati yote na athari yake itakuwa kubwa kote ulimwenguni," amesema.
Alitaja gharama zinazoongezeka, akisema watu tayari wanapambana na kupanda kwa bei za nishati na chakula.
"Wakati Mlango-Bahari wa Hormuz unapomalizwa, maskini zaidi na walio hatarini zaidi duniani hawawezi kupumua," alisema.
Alitoa wito wa mizozo kutatuliwa "kwa amani" na anasema kwamba miundombinu ya raia "ikiwa ni pamoja na mitambo ya nyuklia" inapaswa "kuheshimiwa na kulindwa".
Ameendelea kusema: "Ujumbe wangu uko wazi, kwa Marekani na Israel, ni wakati muafaka wa kusitisha vita vinavyosababisha mateso makubwa ya wanadamu na tayari vimesababisha matokeo mabaya ya kiuchumi."
"Kwa Iran, acheni kushambulia majirani zeni."
Soma zaidi:
Iran yatoa onyo kali, Trump atishia mashambulizi makubwa zaidi
Msemaji wa jeshi la IranEbrahim Zolfaghariamesema kuwa mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya nchi yake hayajakuwa na athari kubwa, akidai kuwa mataifa hayo mawili hayana taarifa kamili kuhusu uwezo wa kijeshi wa Iran.
Amesisitiza kuwa Iran ina vifaa na mikakati ambayo haijafahamika vizuri na wapinzani wake, na hivyo kuonya kuwa hatua yoyote zaidi inaweza kukutana na upinzani mkali.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza, Yvette Cooper, ameanza mazungumzo kuhusu uwezekano wa kufungua tena Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta duniani.
Cooper ameishutumu Iran kwa “uzembe” na kusema kuwa hali ya sasa inahatarisha usalama wa usafirishaji wa kimataifa.
Aidha kwa upande wake rais Donald Trump akihutubia taifa Jumatano jioni, aliwahakikishia Wamarekani kuwa ataimaliza hali hiyo “haraka sana,” ingawa hakutoa muda maalum wa kumaliza mzozo huo.
Kauli yake imezua mjadala kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa na Marekani na athari zake kwa amani na utulivu kimataifa.
Unaweza kusoma pia:Kwa nini ni vigumu kwa Marekani kuchukua madini ya urani ya Iran?
Watoto wanne wauawa kwa shambulio la kisu Uganda
Watoto wanne wameuawa katika shambulio la kisu katika shule moja mjini Kampala, nchini Uganda.
Kwa mujibu wa polisi “Mshukiwa mwenye umri wa miaka 34 amekamatwa, na sababu ya kutekeleza mauaji hayo bado inachunguzwa,” Idara ya polisi ya Uganda imesema kupitia mtandao wa X.
Shule hiyo kwa jina Ggaba Early Childhood Development Program ipo eneo la Makindye katika mji mkuu wa Kampala
Gazeti la Uganda, Daily Monitor, limeripoti kuwa wakazi wa eneo hilo wanasema mshukiwa alisema yeye ni mzazi ili aruhusiwe kuingia shuleni humo, na baada ya kuzungumza na msimamizi wa shule hiyo aliwashambulia watoto hao.
Waathiriwa walikuwa na umri wa kati ya miaka miwili na mitatu, kwa mujibu wa gazeti hilo.
Unaweza kusoma pia;
Mlango Bahari wa Hormuz uko wazi kwa meli ambazo si za “adui”
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran, amesema taifa hilo linaruhusu meli kupita katika mlango bahari wa Hormuz ikiwa “hazimilikiwi na adui wao au kuhusika nao.”
"Mlango Bahari wa Hormuz uko wazi kwa meli ambazo si za “adui”.
Katika mahojiano ya televisheni, Esmail Baghaei anasema meli zinaruhusiwa kupita katika mlango bahari wa Hormuz baada ya ushirikiano na mamlaka ya Iran.
Akiangazia vita vinavyoendelea, msemaji huyo alisema kuwa “Iran haitavumilia kuzungushwa katika mzunguko wa vita, mazungumzo ya kusitisha vita, na makubaliano ya kusitisha vita”
Katika vita kati ya Israel na Iran vilivyodumu siku 12 mwezi Juni mwaka uliopita, Marekani ililenga vituo kadhaa vya kuzalisha nishati ya nyuklia nchini Iran.
“Walisema tuache, tukaacha, na baada ya miezi tisa wameanza tena” alisema Baghaei.
Pia unaweza kusoma :
Raia 1800 wameuawa tangu utawala wa kijeshi kuchukua madaraka Burkina Faso- Ripoti
Zaidi ya raia 1,800 wa Burkina Faso wameuawa tangu kiongozi wa kijeshi Ibrahim Traore kuchukua madaraka miaka mitatu iliyopita na kutekeleza “uhalifu wa kivita na kukiuka haki za kibinadamu” ripoti ya Human Rights Watch inasema.
Ripoti hiyo inaelezea kuwa wa Burkinabe 1,837 wakiwemo watoto waliuawa katika visa 57 kati ya mwezi Januari 2023 na Agosti 2025.
Ripoti hiyo pia inasema mauaji hayo yalitekelezwa na wanajeshi wa taifa hilo, makundi yaliyojihami na makundi yenye itikadi kali.
Human Rights Watch inasema Traore na viongozi wengine sita wa ngazi ya juu ya jeshi “wanapaswa kuwajibishwa kwa maovu waliyotekeleza na kuchunguzwa ikiwemo viongozi watano wa makundi yenye itikadi kali”
Mamlaka za Burkina Faso bado hazijatoa tamko lolote kuhusu ripoti hiyo ya HRW.
Pia unaweza kusoma :
Marekani imemuondelea vikwazo rais wa mpito wa Venezuela Delcy Rodriguez
Hatua hii inakuja chini ya miezi mitatu tangu Marekani kumkamata aliyekuwa rais wa taifa hilo, Nicolas Maduro na mkewe na sasa wanazuiliwa mjini New York wakikabiliwa na mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya.
Rodriguez ambaye ni mshirika wa karibu wa Maduro, na aliyekuwa naibu rais, alikuwa amewekewa vikwazo mwaka 2018 kwa kukandamiza demokrasia.
Aliapishwa kuwa rais baada ya kuidhinishwa na bunge la Venezuela siku chache tu baada ya kukamatwa kwa Maduro.
Kupitia mtandao wa X, Rodriguez alikaribisha hatua hiyo na kusema kuwa “ Ni mwanzo mwema wa kuimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo mawili”
Pia unaweza kusoma :
Trump aziambia nchi zinazotegemea mafuta kutoka Ghuba kuingilia kati mkwamo wa Hormuz
Katika hotuba aliyoitoa hapo jana, rais wa Marekani Donald Trump alizungumzia uzalishaji wa mafuta wa Marekani na Venezuela, na kusema kwamba Marekani haihitaji mafuta kutoka mataifa mengine.
Trump aliyaambia mataifa yanayotumia mafuta kutoka Mashariki ya Kati kuwa yanapaswa kushiriki katika juhudi za kuhakikisha Mlango wa Bahari wa Hormuz unasalia wazi.
Usafirishaji wa mafuta kutoka mataifa ya Ghuba kwa kiasi kikubwa umesitishwa baada ya Iran kujibu mashambulizi ya Marekani na Israel kwa kutishia kushambulia meli zitakazojaribu kuvuka Mlango wa Hormuz ambayo ni njia muhimu katika usafirishaji wa mafuta katika Ghuba ya Uajemi.
Katika hotuba yake Trump alisema kuwa “mataifa ambayo hayawezi kupata mafuta, hayataki kuhusika katika mapambano dhidi ya utawala wa Iran.. Kuweni na ujasiri, nendeni mlango wa bahari wa Hormuz mkaunyakue na kuulinda”Trump aidha alitoa wito kwa mataifa kununua mafuta kutoka Marekani.
Pia unaweza kusoma :
Sekta ya majani chai nchini Kenya yaathirika na vita vya Iran
Usafiri wa bahari Mashariki ya Kati umeathirika kutokana na vita vinavyoendelea Iran, na hii imesababisha zaidi ya kilo millioni 8 za majani chai kusalia katika maghala ya bandari ya Mombasa nchini Kenya, kwa wiki kadhaa, na kuathiri mapato ya wakulima wanaotegemea mauzo ya chai nje ya nchi.
Mkuu wa chama cha wafanyabiashara wa majani chai Afrika Mashariki lenye kusimamia mnada wa majani chai mjini Mombasa, aliiambia shirika la habari la Reuters kuwa kuanzia tarehe 1 mwezi Machi, wamarekodi hasara ya dolla millioni 8 kila wiki.
Mkurugenzi huyo amesema hakuna majani chai yanayosafirishwa kwa sasa kuelekea Mashariki ya Kati ambayo hununua takriban 25% ya mazao ya chai ya Kenya.
Vita vinavyoendelea Iran vimeathiri usafiri wa baharini, huku meli nyingi zikisitisha usafirishaji wa bidhaa kupitia Mlango Bahari wa Hormuz na Bab el-Mandeb.
Kenya huuza zaidi ya kilo millioni 100 ya majani chai Mashariki ya Kati kila mwaka, huku sasa meli zinazopeleka chai katika taifa la Pakistan zikilazimika kutumia njia ndefu ya bahari ambayo ni ghali mno.
Vita vya Ukraine na Urusi pia viliathiri biashara ya majani chai nchini Kenya. Kabla ya vita hivyo, Urusi ilikuwa inaagiza kilo millioni 29 za majani chai kutoka Kenya, ila sasa idadi hiyo imepunguka hadi kilo millioni 5.
Pia unaweza kusoma:
Kiongozi wa kijeshi Libya anunua ndege zisizo na rubani licha ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa
Kiongozi wa kijeshi wa Mashariki mwa Libya, Khalifa Haftar, amenunua kile kinachoonekana kuwa ndege zisizo na rubani za kivita za China na Uturuki, ripoti ya Reuters imebaini, licha ya vikwazo vya muda mrefu vya Umoja wa Mataifa vya kuuzia silaha nchi hiyo iliyogawanyika ya Afrika Kaskazini.
Picha za setilaiti za kibiashara zinaonyesha takriban ndege tatu zisizo na rubani katika kambi ya anga ya Al Khadim, iliyoko jangwani yapata kilomita 100 (maili 62) mashariki mwa jiji la Benghazi, kati ya mwishoni mwa Aprili na Desemba. Kuwasili kwao hakujawahi kuripotiwa hapo awali.
Kile kilichoonekana kama vifaa vya kudhibiti vya ardhini kwa ndege hiyo bado kilionekana mwaka huu, kulingana na wataalamu watatu wa silaha waliopitia picha hizo.
Magari ya angani yasiyo na rubani (UAV) yalichukua jukumu muhimu wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya 2014-2020 nchini Libya, wakati Jeshi la Kitaifa la Libya (LNA) la Haftar lilipojaribu kuipindua serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa huko Tripoli kwa madai kwamba ilikuwa na magenge yenye silaha na "magaidi", jambo ambalo lilikana.
Nchi ikiwa ni pamoja na Falme za Kiarabu (UAE), Misri na Urusi zilitoa uungwaji mkono muhimu kwa Haftar, kulingana na wachunguzi wa Umoja wa Mataifa, huku Uturuki ikiunga mkono utawala wa Tripoli. China iliepuka kuegemea upande wowote.
Makundi yanayopigana ya Libya yalikubaliana kusitisha mapigano mwaka wa 2020, lakini nchi hiyo bado imegawanyika kati ya utawala wa Haftar upande wa mashariki na serikali yenye makao yake makuu Tripoli inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdulhamid Dbeibah upande wa magharibi.
Soma zaidi:
Mashambulizi ya Marekani na Israel 'hayana maana' - Msemaji wa Jeshi la Iran
Msemaji wa jeshi la Iran anasema Marekani na Israel zimekuwa zikilenga shabaha "zisizo muhimu" huku akitishia kufanya mashambulizi "makubwa ya uharibifu" dhidi ya mahasimu wao.
Katika taarifa iliyotolewa kwa shirika la habari la Tasnim na mshirika wa jeshi la Ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) na shirika la habari la Fars, anasema nchi hizo mbili zina taarifa "isiyo kamili" kuhusu uwezo wa zana za kijeshi za Tehran.
Msemaji huyo anaongeza kuwa utengenezaji wa silaha za kijeshi za Iran "unafanyika katika sehemu ambazo huwajui kabisa" - huku akipinga madai ya Trump kwamba hifadhi ya silaha za Iran imepungua sana.
Anasema Marekani na Israel "lazima watalipia uchokozi walioanzisha".
Huku hayo yakijiri msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia anasema nchi hiyo imenasa wimbi jipya la ndege zisizo na rubani.
Anasema ndege nne zisizo na rubani zilinaswa na kuharibiwa.
Hapo awali, wizara hiyo iilitangaza kudondosha kombora la balestiki lililokuwa likielekea eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Soma zaidi:
Milipuko katika ghala la risasi yawaua watu 13 Burundi - jeshi
Takribani watu 13 wamefariki dunia na makumi ya wengine kujeruhiwa katika misururu ya milipuko mikubwa iliyotokea katika ghala la silaha mjini Bujumbura, Burundi, jeshi linasema.
Katika taarifa yake hapo awali ili kwamba watu 57, pamoja na wanajeshi watatu, walijeruhiwa.
Nyumba na magari ya kibinafsi yaliharibiwa, huku vifaa vya kijeshi viliharibiwa katika milipuko hiyo, iliongeza.
Milipuko hiyo ilitokea Jumanne jioni katika kituo hicho, kilicho katika kitongoji cha Musaga, kufuatia hitilafu ya umeme, msemaji wa jeshi alisema hapo awali.
Vipande vya silaha vilivyolipuka vilirushwa zaidi ya kilo mita tano sawa na (maili tatu).
Hapo awali, jamaa za watu walioshuhudia tukio hilo waliiambia BBC kuwa walishuhudia vifo vinne tofauti mjini humo.
Vyanzo vya usalama vililiambia shirika la habari la AFP kwamba makumi ya watu walifariki.
Mwanamke mmoja aliiambia BBC Idhaa ya Maziwa Makuu kwamba jamaa, ambaye alikuwa amezuiliwa katika Gereza Kuu la Mpimba, alifariki baada ya bomu kupiga kituo hicho.
Wafungwa kadhaa waliokuwa katika gereza hilo lililo karibu na ghala la risasi, wameripotiwa kujeruhiwa.
Vita vya Iran: Hotuba ya Trump yatikisa masoko huku bei ya mafuta ikipanda
Bei ya mafuta ilipanda bei na hisa kushuka soko lilipofungulia asubuhi ya Alhamisi barani Asia, kufuatia hotuba ya Rais wa Marekani Donald Trump, ambayo haikuhakikishia masoko ya kimataifa kwamba vita vilikuwa karibu kumalizika na kwamba usafiri wa meli kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz ungerejelea hali ya kawaida.
Mara baada ya Trump kumaliza kuzungumza, bei ya mafuta ghafi ya Brent, ambayo inatathmini kiwango cha kimataifa cha mafuta, ilipanda kwa asilimia tano hadi dola 106 kwa pipa huku masoko ya hisa barani Asia pia yalianza kudorora.
Ijapokuwa Trump alisisitiza ratiba yake ya wiki mbili hadi tatu, hakutoa hakikisho kamili kwa wawekezaji kuhusu jinsi vita hivi vitakavyoisha.
Kauli yake ya kuipiga Iran kwa mabomu na kuirejesha "kurudi Enzi za Kale" ikiwa haitafikia makubaliano imeyumbisha hali ya biashara duniani.
Hata kama mzozo huo utamalizika mwezi huu, bado itachukua muda mrefu kwa viwango vya kawaida vya usafirishaji kuanza tena kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz.
Maelezo zaidi:
Tetemeko la ardhi la ukubwa wa 7.4 lakumba Indonesia
Tetemeko la ardhi la kiwango cha 7.4 limetokea katika Bahari ya Molucca karibu na kisiwa cha Ternate nchini Indonesia mapema Alhamisi na kusababisha kifo cha mtu mmoja.
Tetemeko hilo, ambalo lilitokea saa 06:48 kwa saa za ndani (22:48 GMT) katika kina cha kilomita 35, lilisababisha kutolewa kwa tahadhari ya tsunami ambayo sasa imeondolewa.
Mwanamke mwenye umri wa miaka 70 huko Sulawesi Kaskazini alifariki baada ya kuangukiwa na vifusi vya jengo, na mtu mwingine kuvunjika mguu baada ya kuruka kutoka kwenye jengo, shirika la habari la taifa la Indonesia Antara liliripoti.
Ingawa eneo hilo hukumbwa na viwango vya juu vya mitetemeko ya ardhi, baadhi ya wakaazi wengine waliambia BBC kuwa hili lilikuwa mojawapo ya matetemeko ya ardhi yenye nguvu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka sita iliyopita.
Pia unaweza kusoma:
UAE inazuia makombora yaliyorushwa na Iran
Umoja wa Falme za Kiarabu imekuwa ikikabiliana na vitisho vya kushambuliwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani, wizara yake ya ulinzi ilisema muda mfupi, kabla ya hotuba ya Rais wa Marekani Donald Trump.
Wizara hiyo ilisema mashambulizi hayo yametoka Iran na kuwatahadharisha wananchi wake kuhusu sauti zinazosikika kote nchini wakati ikifanyashughuli ya kuzuia makombora hayo.
Katika hotuba yake kwa taifa kuhusu vita vya Iran hapo awali, Trump aliishukuru UAE na washirika wengine wa Ghuba, ambao wamekosolewa na Iran kwa kulipiza kisasi mashambulizi ya Marekani na Israel.
Trump alisema kuwa utawala wa Iran ulikuwa ukianzisha "mashambulizi ya kigaidi yaliyoharibika" dhidi ya meli za mafuta na nchi jirani ambazo "hazina uhusiano wowote na mzozo huo" alipokuwa akizungumzia wasiwasi kuhusu kupanda kwa bei ya nishati.
Soma pia:
Tazama wakati Artemis iIiporuka angani kwenye safari ya kihistoria
Kwa mara ya kwanza katika zaidi ya miaka 50, binadamu anarudi Mwezini, akisafiri zaidi kutoka duniani kuliko mtu mwingine yeyote aliyewahi kuwa hapo awali.
Kazi hiyo maalumu ya Nasa ya Artemis II, ambayo imezinduliwa usiku wa kuamkia leo imeelezwa kuwa italeta uelewa mpya wa mazingira ya mwezi.
Wanaanga wanne wanafanya safari hii ya kihistoria, baada ya maaandalizi ya miaka kadhaa na hatimaye Mamlaka ya Taifa ya Anga nchini Marekani NASA- kuizindua katka kituo cha anga cha Kennedy Artemis II.
Maelezo zaidi:
Vita vya Iran: Trump asema malengo ya Marekani 'yanakaribia kukamilika'
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema nchi yake imepata mafanikio makubwa katika vita dhidi ya Iran, kufuatia mashambulizi ya pamoja na mshirika wake mkuu, Israel.
Akilihutubia taifa juu ya vita hivyo amesema Marekani itamaliza kazi hiyo na kutishia kushambulia miundombinu ya nishati ya Iran ikiwa viongozi wapya wa nchi hiyo hawatafikia makubaliano.
Katika hotuba hiyo iliyochukua takribani dakika ishirini, Trump amesema mashambulizi dhidi ya Iran, yaliyoanza mwezi mmoja uliopita, yamesababisha uharibifu mkubwa katika vituo vya urutubishaji wa nyuklia nchini Iran, pamoja na kuuawa kwa baadhi ya viongozi wa juu wa serikali hiyo.
Amesisitiza kuwa hatua hizo zimeudhoofisha kwa kiasi kikubwa uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Trump pia amesema kwa zaidi ya miaka 47, Iran imekuwa tishio kwa Marekani na nchi jirani, akitolea mfano jinsi mamlaka ya Tehran ilivyoshughulikia maandamano ya raia wake waliopinga utawala.
Rais huyo amesisitiza kuwa Marekani haitaruhusu Iran kumiliki silaha za nyuklia, akidai kuwa vituo vingi vya urutubishaji wa urani vimeharibiwa vibaya.
Soma zaidi:
Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja leo Alhamisi 02.04.2026