Wanaanga waliosafarini kuzunguka Mwezi wameripotiwa kufikia nusu ya safari hiyo, huku wakichapisha picha za hivi punde zinazonyesha muonekano wa Mwezi kutoka kwa chombo wanachosafiria cha Orion.
Aidha wanaanga hao ambao wametuma ujumbe wa heri njema kwa jamaa zai katika siku ya Jumapili njema, wameonyesha pia jinsi maisha yao yalivyo katika chombo hicho wanachosafiria kwenye safari hii ya kihistoria kufikia upande wa Mwezi ulio mbali zaidi na dunia na jua.
Picha moja inayoiangazia mwezi, ilionyesha pia bonde la Orientale lililo mwezini ambalo linaonekana kwa mara ya kwanza na binadamu, kwa mujibu wa shirika la anga la Marekani – NASA. Hapo awali, mashine aina ya roboti pekee ambazo zimesafiri Mwezini ndizo ambazo zimeweza kupiga picha ya bonde hilo. Bonde hilo linakadiriwa kuwa na upana wa kilomita 965, na inawakilisha eneo la kati kwa umbali kutoka upande ulio mbali zaidi wa Mwezi.
Picha zilizopigwa kutoka kwenye chombo cha Orion, zimeanza kuangazia kwa kina Mwezi , tofauti na awali ambapo chombo hicho kilipiga picha za muonekano wa dunia kama inavyoonekana kutoka kwa anga ya juu. Kwa sasa wanaanga walio katika safari hiyo ya kihistoria wameanza kuangazia Mwezi huku safari hiyo ikifikia mzunguko wa kijivu yaani SILVER ORB.
Wanaanga hao wamesafiri umbali wa nusu ya mwezi kwa sasa na wanatarajiwa kufikiwa kiwango muhimu cha LUNAR FLY BY siku ya Jumatatu ambayo ni katika saa chache zijazo.
Aidha wanaanga hao wamesema kwamba mwezi unazidi kuonekana mkubwa sana wanapouangazia kwenye dirisha za chombo cha Orion wakati ambapo safari yao inaendelea.
Picha za dunia kutoka kwa Artemis II pia zinaendelea kusisimuwa , na zinaonyesha jinsi dunia ilivyo tofauti na unavyoitizama na macho makavu. Picha hizo ni za kwanza kuonekana tangu safari ya kwanza Mwezini.
Wanaanga hao walionekana kwenye matangazo yaliyopeperushwa mubashara , kwenye misheni hiyo wakizungumzia maisha yalivyo kwao katika safari hiyo.
Kwa wakati mmoja, taa zilizimwa ndani ya chombo cha Orion, kuwawezesha waangaanga kutizama vyema yaliyokuwa nje ya chombo hicho.
Na kama ilivyokuwa katika safari ya kwanza ya Artemis 1 iliyofanyika 2022, safari hii ya Artemis II iliwapa wanaanga fursa nafasi ya kupiga picha aina ya SELFIE wakiwa ndani ya chombo hicho kwa kutumia kamera maalum zilizowekwa nje ya chombo hicho . Aidha kamera hizo zina uwezo wa kupiga picha za hali ya juu za Dunia na Mwezi kutoka kwenye anga za juu.
Kuna baadhi ya picha ambazo zimepigwa katika siku ya pili ya safari hiyo ya Artemis II wakati ambapo chombo cha Orion kilikuwa kinapita juu ya dunia.