Moja kwa moja, Watu 200 wafariki baada ya mgodi kuporomoka Mashariki mwa DR Congo

Maporomoko hayo yalitokea katika eneo la Rubaya, ambalo ndilo chanzo kikubwa cha madini ya coltan nchini humo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi na Martha Saranga

  1. Watu 200 wafariki baada ya mgodi kuporomoka Mashariki mwa DR Congo

    xcv

    Chanzo cha picha, Hassan Lali / BBC

    Serikali ya Jamhuri ya demokrasia ya Congo imesema zaidi ya watu 200 wamefariki, wakiwemo watoto 70, baada ya maporomoko ya ardhi mashariki mwa nchi hiyo.

    Maporomoko hayo yalitokea katika eneo la Rubaya, ambalo ndilo chanzo kikubwa cha madini ya coltan nchini humo.

    Tukio hilo lilitokea Jumanne baada ya mvua kubwa kunyesha katika eneo hilo ambalo linadhibitiwa na waasi.

    Katika taarifa ya wizara ya madini ililaumu kundi la waasi la M23, ikisema wanaruhusu uchimbaji wa madini kinyume cha sheria bila kufuata viwango vya usalama.

    Kundi la M23 bado halijatoa kauli yoyote kuhusu tukio hilo. Hata hivyo, chanzo kimoja kutoka Rubaya kiliiambia BBC kuwa kuporomoka huko kwa mgodi kulisababishwa na mashambulizi kutoka kwa majeshi ya serikali, na kwamba watu sita tu ndio waliokufa. Hata hivyo serikali bado haijajibu madai hayo.

    Migodi ya Rubaya inaaminika kuwa na takribani asilimia 15 ya akiba ya coltan duniani, na karibu nusu ya akiba yote ya madini hayo nchini DR Congo.

    Tangu mwaka 2024, waasi wa M23 wamekuwa wakidhibiti eneo la Rubaya, lililoko takribani kilomita 70 magharibi mwa mji wa Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu kaskazini.

    Mamlaka zilisema juhudi za uokoaji baada ya maporomoko ya Jumanne zilikwama kutokana na hali hatari katika eneo hilo. Serikali pia iliilaumu kundi la waasi kwa kuweka vikwazo kwa raia, jambo lililofanya shughuli za uokoaji kuwa ngumu.

    Wizara ya madini iliongeza kuwa kukosekana kwa usimamizi rasmi katika mgodi huo kumewaacha wachimbaji bila ulinzi wa msingi wa usalama kazini.

  2. Askofu mwanaume kutoka Rwanda achaguliwa kuwa kiongozi mpya wa kanisa la Anglikana

    XCV

    Askofu Mkuu Laurent Mbanda wa Rwanda amechaguliwa kuwa kiongozi mpya wa Global Fellowship of Confessing Anglicans (Gafcon), kanisa la Anglikana ambalo halimtambui tena askofu mkuu wa Canterbury kama kiongozi wao mkuu.

    Mbanda kwa sasa ni askofu mkuu wa kanisa la Anglikana nchini Rwanda. Alichaguliwa katika mkutano wa faragha wa baraza la maaskofu wa Gafcon uliofanyika Jumatano usiku, na matokeo yake kutangazwa rasmi Alhamisi.

    Hatua hii inalifanya kanisa la Anglikana, ambalo ni dhehebu la tatu kwa ukubwa kwa upande wa ukristo duniani, kukaribia mgawanyiko mkubwa zaidi kuwahi kutokea.

    Hii inatokea chini ya wiki tatu kabla ya Sarah Mullally kuapishwa rasmi kuwa askofu mkuu mpya wa kanisa la Anglikana.

    Hadi sasa, kanisa la Uingereza pamoja na ofisi ya askofu mkuu wa Canterbury hawajatoa tamko rasmi kuhusu tangazo hilo.

    Uchaguzi huo ulikuwa moja ya matukio makubwa katika mkutano unaoendelea wa Gafcon 26 unaofanyika Abuja, Nigeria.

    Mkutano huo umehudhuriwa na mamia ya wajumbe wa Anglikana wenye msimamo wa kihafidhina kutoka sehemu mbalimbali za dunia, ikiwemo Amerika kaskazini, Australia, na Africa.

    Pia unaweza kusoma:

  3. Iran yadai Marekani na Israeli 'zinalenga maeneo ya raia'

    xcv

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Wizara ya Mambo ya nje ya Iran inaishutumu Marekani na Israeli kwa kulenga maeneo ya raia makusudi kwa mashambulizi yao.

    Kupitia chapisho lake kwenye mtandao wa X, msemaji Esmaeil Baqaei alisema mashambulizi hayo "yanaendelea kuathiri masoko ya kimataifa, yanaongeza bei za nishati, yanavuruga thamani ya sarafu, na kudhoofisha jitihada za watu wa kawaida kote ulimwenguni".

    Aliongeza: "Hata hivyo kwetu sisi Iran, gharama ni kubwa zaidi: watu wetu wanauawa kikatili huku wavamizi wakilenga maeneo ya raia kimakusudi na eneo lolote wanaloamini litasababisha mateso na upotevu wa maisha."

    Donald Trump amesema anatafuta kuharibu uwezo wa makombora ya Iran na uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia.

    Pia unaweza kusoma:

  4. Vyama vya upinzani vya Kikurdi vyakanusha kuingiza wapiganaji Iran

    cvx

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Vyama vya upinzani vya Kikurdi vilivyoko kaskazini mwa Iraq vimekanusha vikali taarifa kwamba baadhi ya wapiganaji wao wamevuka mpaka kuingia Iran.

    “Hii si taarifa ya kweli. Msiiamini,” amesema Hanna Hussein Yazdan Pana kutoka Kurdistan Freedom Party (PAK). “Hakuna hata mpiganaji mmoja wa Peshmerga aliyesogea. Hakuna anayesonga peke yake.”

    Amesema makundi sita ya upinzani ambayo hivi karibuni yameunda muungano yanaratibu mipango yao kwa pamoja, lakini yanahitaji Marekani kwanza kuweka mazingira yatakayoruhusu hatua hiyo. Amesema hakuna kitakachotokea wiki hii.

    “Sio suala la saa au siku,” amesema. “Hatuwezi kusonga mbele kama anga letu halijadhibitiwa. Tunahitaji kuona maghala ya silaha ya utawala yakiharibiwa. Vinginevyo, itakuwa kujitoa mhanga bure.”

    Aidha ametoa wito wa kutenga eneo lisiloruhusu ndege kuruka ili kulinda vikosi vya Wakurdi. “Ulinzi ni mkali sana,” amesema, “na silaha ya juu zaidi tuliyonayo ni bunduki ya Kalashnikov.”

    Tetesi zimeendelea kuongezeka kwamba rais Donald Trump anataka vikosi vya Wakurdi kujiunga na vita ili kupeleka askari wa ardhini. Hata hivyo, Ikulu ya Marekani imekanusha taarifa kwamba anafikiria kuwapa silaha.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Mgawanyiko waongezeka kanisa la Anglikana kuhusu mwanamke kuwa Askofu mkuu wa Canterbury

    xcv

    Chanzo cha picha, PA Media

    Maelezo ya picha, Sarah Mullally alithibitishwa kuwa Askofu Mkuu wa 106 wa Canterbury mwezi Januari

    Makasisi kutoka kundi la kihafidhina la Kanisa la Anglikana wanakutana wiki hii katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, kuchagua mpinzani wa Askofu mkuu wa kwanza mwanamke wa Canterbury.

    Sarah Mullally wa Uingereza atasimikwa rasmi kama kiongozi wa ushirika wa Anglikana duniani katika sherehe ya kifahari baadaye mwezi huu lakini uteuzi wake umepokelewa kwa hisia mseto nchini Nigeria, na kwingineko.

    Wakristo wengi wa kihafidhina wanaamini kwamba wanaume pekee ndio wanaopaswa kuwekwa wakfu kama maaskofu.

    Kanisa Kuu la kihistoria la Vining katika jiji kuu la Nigeria, Lagos, lilifurika wanawake waliovalia "vilemba" vya dhahabu, kijani na zambarau au mitandio ya kufunika vichwa huku wanaume waking'aa katika majoho meupe ya "agbada" kwa ajili ya maadhimisho ya ibada ya Jumapili.

    Baadhi ya nyimbo na liturujia zilikuwa sawa na zile zilizoimbwa na Waanglikana kote ulimwenguni, lakini pia kulikuwa na tofauti, kama vile muziki wa kuabudu wa hali ya juu ambao uliwavutia waumini kucheza kwenye viti vyao.

    Baadhi ya waumini, kama Bunmi Odukoya, waliunga mkono uteuzi huo.

    "Kazi ya Mungu ni jambo la mtu binafsi. Ukiitwa - unaweza kuwa mwanamume, unaweza kuwa mwanamke - unahitaji kutimiza wito wa Bwana," aliiambia BBC.

    Wengine, kama Uche Nweke, hawakukubaliana na hili : "Sidhani kama ni Ukristo. Unapoangalia Biblia na mitume, hakukuwa na mwanamke ndani yake, kwa hivyo mwanamke akiwa mkuu wa kanisa la Anglikana nchini Uingereza, sidhani kama mambo yataenda vizuri."

    Mbali na kuwa kasisi mkuu zaidi katika Kanisa la Uingereza, Askofu Mkuu wa Canterbury pia ni "primus inter pares" - au wa kwanza kati ya walio sawa - wa primate wa Ushirika wa Anglikana duniani kote, ikimaanisha kuwa yeye ni kiongozi wa kiroho wa karibu Waanglikana milioni 95.

    Mbali na kuwa kiongozi mkuu wa Kanisa la Anglikana, Askofu Mkuu wa Canterbury pia ni “primus inter pares” yaani “wa kwanza miongoni mwa walio sawa” miongoni mwa viongozi wakuu wa Kanisa la Anglikana duniani.

    Hii inamaanisha kuwa yeye ni kiongozi wa kiroho wa karibu Waanglikana milioni 95 duniani kote.

  6. Mamlaka ya Hali ya Hewa Kenya yatoa tahadhari ya mafuriko

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Wakenya wameshauriwa kujiandaa kwa mvuu kubwa itakayonyesha katika maeneo tofauti nchini hadi Jumamosi.

    Kulingana na taarifa iliyotolewa kwa umma na Idara ya utabiri wa hali ya hewa mvua itakayozidi milimita 20 itaendelea kunyesha katika maeneo tofauti nchini ndani ya saa 24 zijazo.

    Maeneo yatakayoshuhudia mvua kubwa ni pamoja na Kanda ya Ziwa Victoria, Magharibi mwa Kenya, nyanda za juu na kati pamoja na nyanda za chini kusini.

    Maeneo ya Pwani yanatarajia kupata mvua kubwa hadi tarehe tisa mwezi Machi.

    Wakaazi wa maeneo yaliyotajwa wametahadharishwa kwamba mvua hizo huenda zikasababisha mafurika.

    Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa mafurika yanaweza kushahudiwa hata katika maeneo ambayo hayatakuwa na mvua kubwa.

    Mvua kubwa ikiandamana na nguromo za radi imekuwa ikinyesha katika maeneo tofauti ya nchi katika wiki za hivi karibuni hasa nyakati za usiku.

    Msimu wa mvua wa wa mwezi Machi na Mei umeanza katika maeneo ya Nyanda za Juu Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Victoria, maeneo ya kati mwa nchi na kusini mwa bonde la ufa.

    Wakenya wameombw akuwa makini msimu huu wa mvua na kutoendesha magari katika barabara zilizofurika maji.

    Pia unaweza kusoma:

  7. Uhispania yajibu tishio la Trump la kusitisha biashara kwa 'kupinga vita'

    Pedro Sánchez

    Chanzo cha picha, La Moncloa Handout

    Maelezo ya picha, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez

    Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sánchez amepinga vikali tishio la Rais wa Marekani Donald Trump la kusitisha biashara na nchi hiyo kwa kurejelea msimamo wake dhidi ya vita na kile alichokiita "ukiukaji wa sheria za kimataifa".

    Katika hotuba yake kwa njia ya televisheni ya dakika 10, Pedro Sánchez aliangazia vita vya Ukraine na Gaza, pamoja na Vita vya Iraq zaidi ya miaka 20 iliyopita, na kusema msimamo wa serikali ya Uhispania ni "la kwa vita".

    Trump alitishia kuiwekea vikwazo Uhispania vya kibiashara kwa kukataa ombi la Marekani kutumia vituo vya pamoja vya Moron na Rotafor kuishambulia Iran.

    "Uhspania imekuwa mbaya," Trump alisema wakati wa mkutano na Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz Jumanne.

    "Tutasitisha biashara yote na Uhispania. Hatutaki kufanya lolote naUhispania," aliongeza.

    Merz baadaye alisema kuwa alimwambia Trump waziwazi kwamba angeweza kufanya makubaliano ya kibiashara na Ujerumani au Ulaya yote lakini sio na Uhispania.

    Soma pia:

  8. Qatar yawahamisha wakaazi karibu na Ubalozi wa Marekani mjini Doha

    Qatar

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Qatar imeanza shughuli ya kuwahamisha wakaazi wanaoishi karibu na Ubalozi wa Marekani mjini Doha kama hatua ya tahadhari ya muda, kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Qatar.

    "Malazi yanayofaa yametolewa kwao kama sehemu ya hatua muhimu za tahadhari," Wizara ilisema katika taarifa kwa mtandao wa kijamii wa X.

    Hii inakuja baada ya balozi za Marekani nchini Saudi Arabia na Kuwait, na ubalozi mdogo wa Marekani mjini Dubai, kushambuliwa na ndege zisizo na rubani wiki hii.

    Mapema wiki hii Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitoa witio kwa kwa raia wa Marekani kuondoka haraka iwezekanavya Mashariki ya Kati hata kama safari nyingi za ndege kutoka eneo hilo zimesitishwa au kuahirishwa.

    Serikali ya Marekani imekuwa ikihangaika kutafuta ndege za kukodi kwa raia wa Marekani katika Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia na Jordan, na kutaka kuwasaidia watu waliokwama kwingine kukata tikiti za ndege za kibiashara.

    Afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alisema tangu tarehe 28 Februari, takriban raia 17,500 wamerejea nyumbani kutoka Mashariki ya Kati.

    Maelezo zaidi:

  9. Habari za hivi punde, Iran yakanusha kurusha makombora dhidi ya Uturuki

    Maafisa wakuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wamesema katika taarifa yao kwamba nchi hiyo "inaheshimu mamlaka ya nchi jirani na rafiki yake Uturuki na inakanusha kurusha kombora lolote kuelekea ardhi ya nchi hiyo."

    Wizara ya Ulinzi ya Uturuki ilitangaza jana kuwa kombora la balistiki lililorushwa kutoka Iran lilibadili mkondo kuelekea anga ya Uturuki baada ya kupita katika anga za Iraq na Syria, na kuzuiwa na kuharibiwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa NATO, wenye makao yake mashariki mwa Mediterania.

  10. Tazama: Kiwango cha uharibifu Iran kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel

    Maelezo ya video, Tazama: Kiwango cha uharibifu Iran kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel

    Video zilizorekodiwa kote nchini Iran zinaonyesha milipuko mikubwa katika miji kadhaa huku mgogoro katika eneo hilo ukifikia siku yake ya tano.

    Marekani na Israel ziliishambulia Iran siku ya Jumamosi na kumuua Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei.

    Kanda za video zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii - zilizothibitishwa na BBC na mashirika ya habari - siku chache zilizopita zinaonyesha milipuko na uharibifu mkubwa kote nchini.

    Marekani pia imetoa video ambayo inasema inaonyesha jinsi kambi za kijeshi zilivyopigwa.

    Iran imejibu hatua hiyo kwa wimbi la mashambulizi katika eneo zima la Mashariki ya Kati.

  11. Urusi yaishutumu Ukraine baada ya meli yake kuzama katika bahari ya Mediterania

    Picha ambazo hazijathibitishwa za moto huo ziliwekwa mtandaoni na Mshauri wa Waziri wa Ulinzi wa Ukraine

    Chanzo cha picha, Serhii Sternenko/X

    Maelezo ya picha, Picha ambazo hazijathibitishwa za moto huo ziliwekwa mtandaoni na Mshauri wa Waziri wa Ulinzi wa Ukraine

    Meli ya Urusi ya kusafirisha gesi ya kimiminika (LNG) imezama katika bahari ya Mediterania kati ya Libya na Malta baada ya kukumbwa na mlipuko na kuwaka moto, maafisa wa bandari ya Libya wamesema.

    Urusi imeishutumu Ukraine kwa kuishambulia Arctic Metagaz kwa "ndege zisizo na rubani" zilizorushwa kutoka pwani ya Libya.

    Idara ya usalama ya serikali ya Ukraine SBU haijatoa kauli yoyote kuhusiana na madai hayo huku mamlaka ya bandari ya Libya imesema chanzo cha moto kwenye meli hiyo hakijabainika.

    Raia wa Libya wanasema meli hiyo ilikuwa imebeba takriban tani 62,000 za LNG kabla ya kukumbwa na milipuko na kwamba ilizama takriban maili 130 (240km) kaskazini mwa bandari ya Sirte nchini Libya.

    Wizara ya uchukuzi ya Urusi ilisema Warusi 30 walikuwa ndani ya Arctic Metagaz.

    Waziri wa Mambo ya Ndani wa Malta Byron Camilleri alisema wote walipatikana wakiwa "salama katika boti ya uokozi" wakati wa operesheni ya uokoaji ya vikosi vya jeshi vya Malta.

    Picha ambazo hazijathibitishwa zilizoibuka mitandaoni zinaonekana kuonyesha meli hiyo ikiwaka moto baada ya shambulio hilo la Jumanne.

    Maelezo zaidi:

  12. Zelensky tayari kuzisaidia nchi za Ghuba kukabiliana na mashambulizi ya droni

    Volodymyr Zelensky

    Chanzo cha picha, EPA

    Maelezo ya picha, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky

    Rais Volodymyr Zelensky amesema kwamba Ukraine inaandaa mipango ya kupeleka wataalamu katika eneo la Ghuba kusaidia washirika walinda nchi zao dhidi ya ndege zisizo na rubani na makombora ya Iran.

    Anasema alizungumza na wenzao katika Falme za Kiarabu UAE na Qatar hapo jana, na Jordan na Bahrain hii leo.

    Baada ya kujadili mzozo wa Mashariki ya Kati na mawaziri na makamanda, aliwaomba kubuni mkakati wa kuwasaidia washirika - bila kudhoofisha ulinzi wa Ukraine yenyewe.

    Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X, Rais Zelensky alisema: "Ukraine inaweza kusaidia kulinda maisha na kuleta utulivu..."

    Aliongeza: "Jeshi letu lina uwezo unaohitajika. Wataalamu wa Ukraine watafanya kazi mashinani, na timu tayari zinaratibu hili. Tuko tayari kusaidia kulinda maisha, kulinda raia, na kuunga mkono juhudi za kweli za kuleta utulivu wa hali hiyo na kurejesha urambazaji salama katika eneo hilo."

    Soma pia:

  13. EPL: Arsenal yatamba, City wapata sare huku Man United ikipoteza

    .

    Chanzo cha picha, Reuters

    Arsenal walinusurika pambano kali dhidi ya Brighton na kuendeleza uongozi wao kileleni mwa Ligi ya Premia hadi pointi saba.

    Brighton walikuwa timu bora kwa muda mrefu - lakini bao la Bukayo Saka lililofungwa mapema lilitosha kukipa kikosi cha Mikel Arteta ushindi wa hali ya juu huku wapinzani wao Manchester City wakilazimishwa sare ya 2-2 nyumbani na Nottingham Forest.

    Usiku wa Arsenal nusura uanze kwa njia ya janga katika sekunde za mwanzo wakati kipa David Raya alipompatia mpira kimakosa Carlos Baleba, lakini jaribio lake la kupangua lilikuwa dhaifu, na kumruhusu Gabriel kurudi nyuma na kuokoa shambulizi lake.

    Baadaye bahati ya The Gunners ilisimama baada ya dakika tisa wakati shuti la kawaida la Saka lilipomtoka Baleba na kupita kwenye miguu ya kipa wa Brighton Bart Verbruggen, ambaye hakuwa na jibu.

    Wakati huohuo Nattingham ambao walikuwa wanacheza ugenini dhidi ya Man City walikaa nyuma na kulinda lango la huku City ikitawala katika kipindi kirefu cha mchezo kabla ya Antoine Semenyo kufunga bao la kwanza na kutoa onyo kwa wageni.

    Wenyeji waliweka presha yao baada ya nusu saa wakati Rayan Cherki alipozamisha krosi ndani ya eneo la hatari na aliyesajiliwa Januari Semenyo akafunga bao lake la saba tangu ajiunge na City.

    Vilevile Manchester United ililazimika kukubali matokeo baada ya kufungwa 2-1 na wachezaji 10 wa Newcastle ugenini.

    Hatahivyo Michael Carrick hakuitupa timu yake tofauti na mtangulizi wake Ruben Amorim ambaye mara nyengine alinukuliwa akisema : "hii labda ni timu mbaya zaidi katika historia ya Manchester United", wakati alipokuwa akitoa maoni hayo zaidi ya mwaka mmoja uliopita baada ya kushindwa nyumbani na Brighton.

    Lakini Carrick anajua siku 11 kati ya kichapo cha 2-1 kutoka kwa Newcastle katika uwanja wa St James' Park na ziara ya Aston Villa Old Trafford mnamo Machi 15 zinaweza kuwa muhimu zaidi msimu wake.

    Pia unaweza kusoma:

  14. Hezbollah 'haitajisalimisha' asema kiongozi wake huku mashambulizi ya Israel yakiongezeka

    Kiongozi wa Hezbollah Naim Qassem pichani Julai 2024

    Chanzo cha picha, Anadolu via Getty Images

    Maelezo ya picha, Kiongozi wa Hezbollah Naim Qassem

    Kiongozi wa Hezbollah Naim Qassem amesema Kundi hilo linaloungwa mkono na Iran "halitajisalimisha" huku vita na Israel vikiendelea kuongezeka.

    Katika hotuba yake ya kwanza ya hadhara tangu mzozo wa kikanda kuenea nchini Lebanon siku ya Jumatatu, Qassem alisema Hezbollah ilizingatia makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mwishoni mwa 2024, lakini Israel "haikuzingatia masharti yake yoyote".

    "Tulikubaliana na suluhisho la kidiplomasia tukiliona kuwa ni fursa kwa serikali kuchukua jukumu lake, lakini tumekuwa tukisema mara kwa mara 'kuna mipaka ya uvstahamilivu'," alisema katika hotuba ya runinga.

    "Chaguo letu ni kukabiliana nao hadi kufikia hatua ya kujitolea kabisa, kwa mipaka ya mbali zaidi, na hatutasalimu amri," alisema.

    Hezbollah ilirusha roketi na ndege zisizo na rubani kuelekea Israel siku ya Jumatatu baada ya Kiongozi Mkuu wa Iran Ayotollah Ali Khamenei kuuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel.

    Israel imejibu mashambulizi ya anga na kupeleka wanajeshi kusini mwa Lebanon, huku maelfu ya raia wakilazimika kutoroka makaazi yao.

    Maelezo zaidi:

  15. Bunge la Seneti la Marekani lashindwa kudhibiti mamlaka ya vita ya Trump dhidi ya Iran

    .

    Chanzo cha picha, Getty Images

    Azimio la pande mbili linalolenga kudhibiti uwezo wa Rais Donald Trump wa kuanzisha vita nchini Iran limeshindwa katika Bunge la Seneti la Marekani, huku mgogoro ukiendelea kuongezeka Mashariki ya Kati.

    Hatua ya mamlaka ya vita ilikataliwa kwa kura 53 dhidi ya 47 ambayo kwa kiasi kikubwa kilipigwa kwa misingi ya chama. Ingesitisha hatua za kijeshi za Marekani nchini Iran bila idhini ya bunge.

    Wabungue wa chama cha Democratic wanasema kuwa Trump alichukua hatua ya kuishambulia Iran bila idhini ya Congress kwa kutoa sababu zinazobadilika za vita. Baadhi ya wa Republican wanasema watazuia azimio hilo, lakini wanaweza kubadilisha msimamo wao ikiwa vita vitaongezeka.

    Huku hayo yakijiri Jeshi la Israel limefanya mashambulizi mengine dihdi ya mkuu wa Iran Tehran.

    "IDF imeanza wimbi la ziada la mashambulizi yanayolenga miundombinu ya kijeshi ya utawala wa Iran kote Tehran," Jeshi la Ulinzi la Israel linasema katika taarifa.

    Jeshi hilo halikutoa maelezo zaidi kuhusu eneo mahususi, lakini inasema maelezo zaidi yatafuata.

    Shirika la habari la AFP linaripoti kuwa waandishi wake walishuhudia mlipuko mkubwa katika mji mkuu Jumatano usiku.

    Hapo awali, jeshi la Israel lilitangaza kuwa jeshi lake la anga lilikuwa limekamilisha "mashambulio makubwa" dhidi ya kambi ya mashariki ya Tehran yenye vituo vya amri na maafisa wa usalama wa ndani.

    Soma zaidi:

  16. Karibu katika matangazo ya moja kwa moja.

Trending Now