Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Ndege ya kivita ya Marekani yadunguliwa katika anga la Iran

Shirika la habari la Iran la Tasnim linadai kuwa Marekani inamtafuta mmoja wa marubani wake; BBC imewasiliana na Kamandi Kuu ya Marekani kwa maoni.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi & Asha Juma

  1. Israel yasitisha mashambulizi katika eneo la utafutaji marubani nchini Iran - ripoti

    Jeshi la Israel limeahirisha mashambulizi katika eneo la Iran ambapo utafutaji wa marubani wa ndege za kivita za Marekani unaendelea, kulingana na ripoti kutoka CNN, shirika la habari la AP na Channel 12 ya Israeli.

    CNN inasema afisa wa Israeli alisema kwamba mashambulizi yameahirishwa katika eneo la utafutaji, huku Channel 12, ikimnukuu afisa mkuu wa Israel, ikiripoti kwamba mashambulizi yote yamesitishwa. AP pia iliripoti kwamba mashambulizi ya angani yamesitishwa katika maeneo husika kutokana na juhudi za uokoaji.

    AP inasema afisa huyo wa Israeli alizungumza nao kwa sharti la kutotajwa jina "kwa sababu operesheni hiyo inaendelea".

    Jeshi la Ulinzi la Israeli halijathibitisha ripoti hizi.

    Soma zaidi:

  2. Picha zinaonekana kuonyesha mabaki ya ndege aina ya US F-15E

    BBC Verify imezungumza na mtaalamu ambaye amethibitisha kwamba picha ya mabaki zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii ni ya ndege aina ya US F-15E Strike Eagle.

    Kipande kinachoonyeshwa ni ncha bawa na sehemu ya kiimarishaji wima ya ndege kutoka Kikosi cha Wapiganaji cha Marekani cha 494 kilichoko RAF Lakenheath nchini Uingereza, kulingana na Justin Bronk, mtafiti mkuu wa anga na teknolojia katika timu ya Sayansi ya Kijeshi.

    Uchunguzaji wa picha kinyume kinyume unaonyesha picha hizo zilianza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii hii leo.

    Hatuwezi kuthibitisha mahali ambapo picha zilipigwa kwa sababu ni za karibu sana na hakuna ishara dhahiri inayoturuhusu kuzipata katika eneo la kijiografia, lakini tumeziangalia kwa teknolojia ya akili mnemba na hakuna dalili zinazoonyesha kuwa ni za uwongo.

    Soma zaidi:

  3. Tunachojua kufikia sasa kuhusu taarifa za kudunguliwa kwa ndege ya Marekani na Iran

    Bado chumba chetu cha habari kinaendelea kupokea taarifa zinazohusiana na ndege ya kivita ya Marekani iliyodunguliwa juu ya anga la Iran.

    Tunachojua:

    • Ndege ya kivita ya F-15E imeripotiwa kudunguliwa kusini mwa Iran
    • Rubani mmoja wa ndege hiyo ameokolewa na vikosi vya Marekani, kulingana na mshirika wa BBC wa Marekani CBS - ndege ya F-15E kwa kawaida huwa na marubani wawili
    • Rais wa Marekani Donald Trump amearifiwa kuhusu tukio hilo, kulingana na Waziri wa Habari wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt
    • Vyombo vya habari vya Iran vinaripoti kwamba mamlaka imeahidi kutoa zawadi ya bilioni 10 za tomani (karibu pauni 50,000) kwa yeyote atakayemkamata rubani wa Marekani akiwa hai.

    Tusichokijua:

    • Ingawa rubani mmoja ameripotiwa kuokolewa, hakuna taarifa yoyote kuhusu mwingine
    • Mazingira yaliyozunguka kudunguliwa kwa ndege hiyo bado hayajabainika wazi
    • Bado Trump hajazungumza lolote

    Soma zaidi:

  4. Israel yaanzisha mashambulizi zaidi mjini Tehran na Beirut

    Wakati shughuli ya kutafuta ndege ya Marekani iliyodunguliwa na Iran ikiendelea, Israel imeanzisha mashambulizi dhidi ya Iran na Lebanon.

    Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema limeanzisha wimbi jingine la mashambulizi mjini Tehran.

    Katika saa 24 zilizopita, IDF inasema imetekeleza “zaidi ya mashambulizi 70 katika maeneo ya magharibi na katikati mwa Iran yakilenga vituo vya kurushia makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani.”

    IDF pia inasema imeanzisha mashambulizi katika maeneo tofauti mjini Beirut na wamedungua makombora kadhaa yaliyorushwa na Iran.

    Pia unaweza kusoma:

  5. Spika wa Iran akejeli Marekani baada ya ndege yao kudunguliwa

    Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, ameikejeli Marekani kupitia mtandao wa kijamii wa X, baada ya taarifa kwamba ndege ya kivita ya Marekani kudunguliwa na Iran.

    “Baada ya kuishinda Iran mara 37 mfululizo, vita hivi vya kipuuzi visivyo na mkakati wowote walivyovianzisha wenyewe sasa vimewashusha hadhi kutoka kutaka ‘kubadilisha utawala’ hadi ‘kuna mtu anaweza kuwatafuta marubani wetu? Tafadhali?’,” Ghalibaf aliandika kwenye ukurasa wake wa X.

    Tarehe 31 mwezi Machi, Rais Trump alisema kuwa kumekuwa na mabadiliko ya utawala nchini Iran, na kuongezea kuwa viongozi wapya wa Iran “hawana misimamo mikali sana.”

    Ghalibaf pia aliandika kwa kejeli, ."Hii ni hatua nzuri sana. Hiki ni kitu cha kipekee."

    Ukurasa was spika huyo umekuwa ukichapisha mambo mengi siku za hivi karibuni, ikijumuisha picha na video za kejeli huku mara ya mwisho kuonekana kwenye televisheni ikiwa ni Machi 17.

    Taarifa ambazo hazijadhibitishwa zinasema kuwa Marekani ilikuwa inamuona Ghalibaf kuwa na uwezo wa kuwa mshirika wao siku za mbeleni.

    Soma zaidi:

  6. Hii ni mara ya kwanza ndege ya Marekani kudunguliwa na Iran katika vita hivi

    Hii ni mara ya kwanza kwa ndege ya kivita ya Marekani kudunguliwa katika anga la Iran tangu kuanza kwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.

    Ndege tatu za F-15E zilidunguliwa mapema vita vilipoanza kwa kile walichokiita “mashambulizi ya kimakosa na Kuwait”

    Tukio hili lina maanisha nini?

    Kwanza, linakuja baada ya Donald Trump na Waziri wake wa ulinzi Pete Hegseth mara kadhaa kudai kuwa Marekani kimsingi imeshinda vita hivi.

    Hegseth pamoja na makamanda wa kijeshi wamezungumzia “ubabe wa anga” wa Marekani na jinsi ambavyo wameidhoofisha Iran.

    Trump pia amewahi kudai kuwa, Iran “haiwezi kufanya chochote” dhidi ya ndege za Marekani zinazopitia kwenye anga lake.

    Kauli hizo sasa zinaonekana kuwa za kujiamini kupita kiasi. Tukio hili linaonyesha kuwa Iran bado ina uwezo fulani wa kijeshi ingawa huenda ni mdogo sana wa kulinda anga zake dhidi ya mashambulizi.

    Pili, tukio hili linakuja wakati ambapo Marekani imekuwa ikitishia kuongeza mashambulizi yake dhidi ya Iran iwapo makubaliano ya haraka hayataafikiwa.

    Tukio hili linaweza kuchochea mashambulizi Zaidi za kulipiza kisasi kutoka Marekani.

    Pia linaweza kuongeza wasiwasi miongoni mwa raia wa Marekani kwamba wanajeshi wao zaidi wanaathiriwa na vita hivi, hasa wakati ambapo utawala wa Trump unatarajiwa kufanya uvamizi wa ardhini nchini Iran - ambayo itaongeza hatari kwa wafanyikazi wa Marekani kwa kiasi kikubwa.

    Soma zaidi:

  7. Habari za hivi punde, Rubani mmoja wa ndege ya kivita ya Marekani aokolewa - Maafisa

    Maafisa wawili wa Marekani wameiambia CBS News kwamba rubani mmoja wa ndege ya kivita ya F-15 iliyodunguliwa ameokolewa.

    Kulingana na maafisa, mfanyakazi huyo ameokolewa na vikosi vya Marekani.

    Trump aarifiwa kuhusu ndege ya Marekani iliyoanguka - Ikulu ya Marekani yathibitisha

    Rais wa Marekani Donald Trump amepewa taarifa kuhusu ndege ya kivita ya Marekani iliyoanguka juu ya anga la Iran, kulingana na Katibu wa Habari wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt.

    "Rais amepewa taarifa," amesema.

  8. Video inayoonyesha jinsi Marekani inavyotafuta ndege yao iliyodunguliwa na Iran

    BBC Verify imethibitisha video inayoonyesha kile kinachoonekana kuwa ndege ya Marekani ikiwa imeambatana na helikopta mbili zikipaa kusini mwa Iran huku shughuli ya uokoaji ikiendelea kutafuta marubani wa ndege ya Marekani iliyodunguliwa na Iran.

    BBC imethibitisha kuwa video hiyo ilichukuliwa katika mkoa wa Khuzestan, karibu na daraja lililoko juu ya mto Karun.

    Video hiyo imethibitishwa na BBC kwa uangalifu ili kuhakikisha ni ya hivi karibuni na haijatengenezwa na akili mnemba.

    Ripoti kutoka Marekani, zinasema operesheni ya kuwatafuta marubani wa ndege hiyo inaendelea baada ya kudunguliwa na Iran.

    BBC Verify inaendelea kukagua picha na video zinazoonyesha oparesheni hiyo ilivyofanyika.

    Soma zaidi:

  9. Iran yathibitisha kifo cha mkuu wa ujasusi wa jeshi la wanamaji

    Jeshi la Iran (IRGC) limethibitisha kifo cha Behnam Rezaei, mkuu wa Idara ya Ujasusi ya Jeshi la Wanamaji la kikosi cha IRGC.

    Israel hapo awali ilitoa taarifa kuwa ilimlenga Rezaei katika shambulizi walilotekeleza tarehe 26 Machi.

    “Rezaei alikuwa na jukumu la kukusanya taarifa za kijasusi kuhusu nchi za kanda na aliongoza ushirikiano na mashirika mbalimbali ya ujasusi,” lilisema jeshi la Israel (IDF).

    Vyombo vya habari vya Iran viliripoti kufanyika kwa mazishi Rezaei tarehe 27 Machi, lakini sasa jeshi la IRGC limethibitisha kifo chake siku kadhaa baada ya tukio hilo.

    Tarehe 26 Machi, Israel pia ilisema ilimuua kamanda wa jeshi la wanamaji la IRGC, Alireza Tangsiri, ambaye alikuwa akisimamia kufungwa kwa njia muhimu ya Mlango Bahari wa Hormuz. IRGC ilithibitisha kifo cha Tangsiri siku nne baada ya Israel kutangaza.

    Pia unaweza kusoma :

  10. Habari za hivi punde, Ndege ya kivita ya Marekani yadunguliwa juu ya anga la Iran - Vyombo vya habari

    Ndege ya kivita ya Marekani imedunguliwa juu ya anga la Iran, huku shughuli ya kutafuta wafanyakazi wake ikiendelea kwa sasa, afisa mmoja wa Marekani ameambia Axios, shirika la habari la Reuters na New York Times.

    Vile vile, Wall Street Journal inaripoti kwamba Marekani inafanya operesheni ya uokoaji kutafuta wafanyakazi hao.

    Shirika la habari la Tasnim, ambalo lina uhusiano na jeshi la IRGC, linadai kuwa Marekani inamtafuta mmoja wa marubani wake.

    Kituo kikuu cha oparesheni za kijeshi Marekani Centcom, kilikanusha taarifa za IRGC kwamba rubani wa ndege ya kivita alikuwa ameshambuliwa katika kisiwa cha Qeshm, katika Mlango Bahari wa Hormuz

    Shirika la habari la Tasnim linaripoti kuwa helikopta za Marekani, na ndege zisizo na rubani za upelelezi zinamtafuta rubani huyo katika eneo hilo karibu na Mlango Bahari wa Hormuz.

    Televisheni ya kitaifa ya Iran imesema kuwa itatoa zawadi kwa yeyote atakayemkamata rubani huyo akiwa hai.

    BBC haijathibitisha madai haya na inaendelea kukusanya taarifa zaidi.

    Pia unaweza kusoma :

  11. Raia wote Afrika kuzuru Ghana bila viza

    Rais wa Ghana, John Mahama, amesema taifa lake, litazindua mfumo wa kutoa viza ya kuingia nchini humo kuwa bure kwa mataifa yote ya bara Afrika kuanzia mwezi Mei tarehe 25.

    Rais huyo alitoa tangazo hilo baada ziara ya rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa nchi humo.

    Tarehe 25 mwezi Mei itaendana na siku ya Afrika ambayo husherehekewa nchini humo kuadhimisha utamaduni na historia ya kiafrika.

    “Viza ya bure kwa waafrika itakuwa sehemu ya sera mpya ya viza ya kielektroniki ya utawala wa mahama” Alichapisha ujumbe huo kwenye mtandao wa X, Waziri wa mambo ya kigeni wa Ghana Samuel Ablakwa.

    Mwaka 2024, Rais wa zamani Nana Akufo-Addo alitangaza kwa mara ya kwanza sera ya viza ya bure kwa wamiliki wa pasipoti za Afrika kuanzia Januari 2025.

    Hata hivyo, waziri wa mambo ya nje alifafanua kuwa sera hiyo haikuweza kuanza kutekelezwa kwa sababu mifumo na hatua za usalama hazikuwa bado zimewekwa.

    Pia unaweza kusoma :

  12. Israel imeharibu 70% ya uzalishaji wa chuma wa Iran - Netanyahu

    Mashambulizi ya Israel yameharibu takriban 70% ya uwezo wa uzalishaji wa chuma wa Iran, amesema Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.

    Katika video iliyochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, Netanyahu amesema haya ni "mafanikio makubwa" ambayo yanainyima jeshi la Iran (IRGC) rasilimali za kifedha na kijeshi.

    "Kwa ushirikiano kati yangu na Rais Donald Trump, kati ya jeshi la Israel IDF na jeshi la Marekani, tutaendelea kuisambaratisha Iran," ameongezea kuwa Israel itaendelea kushambulia kundi la Hezbollah.

    Pia unaweza kusoma :

  13. Marekani inaweza kufungua Mlango Bahari wa Hormuz ikipewa muda kidogo – Trump

    Rais Donald Trump amesema Marekani inaweza kufungua Mlango Bahari wa Hormuz ikipatiwa muda zaidi kidogo, huku shinikizo likiongezeka kwa utawala wake kupata suluhisho la haraka la vita dhidi ya Iran.

    Trump amesema hayo kupitia ujumbe kwenye tovuti yake ya mitandao wa Truth Social.

    Aliandika: "Muda kidogo zaidi, tunaweza kufungua kwa urahisi NJIA YA HORMUZ, KUCHUKUA MAFUTA, NA KUPATA UTAJIRI. IITAKUWA MAFUTA 'MENGI' KWA DUNIA???"

    Trump ametoa maoni tofauti mara kwa mara kuhusu jinsi Mlango-Bahari unavyoweza kufunguliwa tena, akidokeza kwamba mataifa ya Magharibi yanapaswa kuhakikisha kuwa usambazaji wa mafuta unapita katika eneo muhimu kwa kutumia njia za kijeshi.

    Iran imefunga kwa ufanisi Mlango wa Hormuz, njia muhimu ya usafiri wa majini duniani kote, kulipiza kisasi mashambulizi ya Marekani na Israeli yaliyoanza mwishoni mwa Februari.

    Soma zaidi:

  14. Burkina Faso lazima 'isahau' kuhusu demokrasia - Kiongozi wa Kijeshi asema

    Demokrasia "inaua" na watu wa Burkina Faso lazima "wasahau" hili, Rais wa kijeshi wa nchi hiyo amesema katika mahojiano yaliyorushwa hewani kwenye televisheni ya serikali.

    Kapteni Ibrahim Traoré, ambaye alichukua madaraka katika mapinduzi ya kijeshi miaka mitatu iliyopita, alisemaa kwamba Waafrika wengi hawataki mfumo wa demokrasia na kwamba Burkina Faso ilikuwa na mbinu yake mbadala, bila kutoa maelezo zaidi.

    Awali, Traoré aliahidi kurejesha utawala wa kidemokrasia katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi ifikapo Julai 2024, lakini miezi miwili kabla ya tarehe hii ya mwisho, utawala wa kijeshi ulitangaza kwamba utaongeza utawala wake kwa miaka mingine mitano.

    Miezi miwili iliyopita, mamlaka zilitangaza kupiga marufuku vyama vyote vya siasa kama sehemu ya mpango wa "kujenga upya taifa hilo".

    Katika mahojiano ya Alhamisi usiku, Traoré alisema: "Watu wanahitaji kusahau kuhusu suala la demokrasia. Demokrasia si yetu."

    "Tazama Libya, huu ni mfano unaotukaribia," alisema rais huyo mwenye umri wa miaka 38.

    Libya ilitawaliwa kidemokrasia kwa miongo minne na Kanali Muammar Gaddafi, ambaye alisimamia utawala wa ukatili huku pia akiwapa Walibya ruzuku ya makazi, elimu ya bure na huduma ya afya ya bure.

    Aliuawa wakati wa uasi uliosaidiwa na uingiliaji kati wa kijeshi wa Magharibi. Tangu wakati huo, nchi hiyo ya Afrika Kaskazini imeshindwa katika dhamira yake ya kuanzisha demokrasia na badala yake imegawanyika kati ya tawala mbili hasimu.

    Soma zaidi:

  15. Kiwanda cha kusafisha mafuta cha Kuwait chashambuliwa kwa mara ya tatu

    Baada ya kushambuliwa na ndege zisizo na rubani nyingi asubuhi ya Ijumaa, moto ulizuka katika sehemu za kiwanda muhimu cha kusafisha mafuta huko Kuwait.

    Hakuna majeraha walioripotiwa.

    Kiwanda cha kusafisha mafuta cha Mina al-Ahmadi, ambacho ni mojawapo ya vikubwa zaidi Mashariki ya Kati, kinaweza kusafisha hadi mapipa 346,000 ya mafuta kwa siku.

    Kuwait ina viwanda vitatu vikubwa vya kusafisha mafuta. Kiwanda chake cha kusafisha mafuta cha Mina al-Ahmadi kimekuwa kikilengwa na ndege zisizo na rubani za Iran mara mbili hapo awali wakati wa mzozo wa wiki tano.

    Shirika la Petroli la Kuwait linasema timu za dharura na zimamoto zimekuwa zikifanya kazi ya kudhibiti moto katika baadhi ya vitengo 39 vya kiwanda cha kusafishia mafuta na kuzuia kuenea kwake.

    Inaongeza kuwa ubora wa hewa katika eneo lililoathiriwa unafuatiliwa, na kwamba hadi sasa hakuna athari yoyote kwenye mazingira ya eneo hilo.

    Maafisa wanasema Iran yashambulia kiwanda cha kuondoa chumvi kwenye maji Kuwait

    Wizara ya Umeme na Maji ya Kuwait imesema kiwanda cha kuondoa chumvi kwenye maji kimeshambuliwa na Iran, na kusababisha "uharibifu wa vifaa".

    Timu za kiufundi na za dharura zilianza kazi "mara moja" ili "kudumisha ufanisi wa uendeshaji", inasema katika taarifa kwenye mtandao wa X.

    "Usalama na uthabiti wa mfumo wa umeme na maji ni kipaumbele cha juu," taarifa hiyo inaongeza.

    Soma zaidi:

  16. Macron akosoa mwenendo wa Trump katika vita vya Iran

    Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema vita vya Iran vinahitaji kushughulikiwa kwa kuzingatia msimamo"imara", ambao haubadiliki kila uchao.

    Macron ambaye yuko ziarani nchini Korea Kusini, aliwaambia waandishi wa habari kwamba "hili sio onyesho. Tunazungumzia vita, amani na maisha ya watu".

    "Hufai kubadilisha kauli kila wakati," anasema, akionekana kuashiria ujumbe unaokinzana unaotolewa na utawala wa Trump kuhusu vita vya Iran.

    Utawala wa Trump umedokeza kwa nyakati tofauti kuwa usitishaji mapigano unakaribia, ukisistiza kuwa malengo yake ya vita nchini Iran yamefikiwa kabla ya msimamo huo kubadilishwa kuwa Marekani itaendelea kupigana.

    "Nadhani hupaswi kuongea kila siku. Unapaswa kuacha mambo yatulie," aliongeza kusema Macron.

    Maelezo zaidi:

  17. Vita vya Iran: Bei ya mafuta yatarajiwa kupanda Kenya

    Wakenya wametahadharishwa kuwa bei ya mafuta huenda ikapanda, huku athari za vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati zikianza kushuhudiwa.

    Bei ya bidhaa hiyo muhimu duniani imekuwa ikipanda, na serikali sasa haina budi kushughulikia hali hiyo alisema Waziri wa Fedha John Mbadi.

    Kuanzia katikati ya mwezi Aprili, bei ya mafuta huenda ikakabiliwa na shinikizo kuongezaka. Hata hivyo, Waziri Mbadi anasema mabilioni ya fedha zitatumika kupunguza athari ya kupanda kwa bei ya mafuta kwa watumiaji, lakini kwa muda mfupi tu.

    "Mzunguko wa sasa wa bei ya mafuta, Machi 15, 2026, hadi Aprili 14, 2026, hauwezi kuathiriwa kwa vile bidhaa husika ilitolewa kabla ya mzozo wa Mashariki ya Kati," alisema Mbadi.

    Serikali, hata hivyo, inasema kuwa takriban Ksh.17 bilioni zinazoshikiliwa kwa sasa katika hazina ya uimarishaji chini ya Ushuru wa Maendeleo ya Petroli zitatumwa ili kudhibiti bei na kuwakinga watumiaji kutokana na ongezeko kubwa kwa muda wa miezi mitatu ijayo.

    Serikali pia inafikiria kusitisha utozaji wa ushuru wa ziada (VAT) wa mafuta, kama hatua ya kudhibiti bei ya ya bidhaa hiyo.

    Pia unaweza kusoma:

  18. Wakenya 16 hawajulikani waliko baada ya kujiunga na jeshi la Urusi

    Wakenya 16 wametoweka nchini Urusi baada ya kujiunga na jeshi la nchi hiyo, na wengine 47 wamerejea nyumbani kutoka vitani nchini Ukraine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi ameimbia kikao cha kamati ya Bunge la Seneti.

    Wengine 38 kwa sasa wako katika hospitali tofauti za Urusi chini ya vizuizi vya ufikiaji Mudavadi aliongeza kusema.

    Idadi ya Wakenya waliotoweka nchini Urusi imeongezeka kutoka 10 hadi 16 ndani ya saa 24 zilizopita.

    Bado haijabainika ikiwa wamefariki au wako hai.

    Waziri huyo pia alikadiria kuwa Wakenya 165 wanashiriki kikamilifu katika operesheni za kijeshi, na kufanya jumla ya walioshiriki katika mzozo wa Ukraine kufikia zaidi ya 250.

    Mudavadi alisema idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi.

    Aliongeza kuwa Wakenya wawili wanazuiliwa nchini Ukraine kama wafungwa wa kivita.

    Mudavadi pi alisema walioajiriwa wametia saini kandarasi za kuhudumu kama maafisa wa usafirishaji au kufanya majukumu ya kivita.

    "Kinyume na ripoti zilizopo, Wakenya wengi walijiunga na jeshi la Urusi kwa hiari," Mudavadi aliambia kamati ya wabunge.

    Baadhi ya mashirika yenye makao makuu nchini Kenya, Urusi, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu yalihusika na usajili huo, kwa mujibu wa waziri Mudavadi.

    Kenya imeanzisha uchunguzi kuhusu usajiliwa kwa raia wake kupigana vita nchini Ukraine kinyume cha sheria.

    Soma zaidi:

  19. Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth amtaka Mkuu wa Majeshi kuachia ngazi

    Waziri wa Ulinzi wa Marekani Pete Hegseth amemtaka Mkuu wa Majeshi Randy George kuachia wadhifa wake, kulingana na CBS News, mshirika wa habari BBC wa Marekani.

    Msemaji Mkuu wa Pentagon Sean Parnell alisema katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii kwamba George "atastaafu kutoka wadhifa wake kama Mkuu wa 41 wa Wanajeshi mara moja".

    Mkuu wa Jeshi kawaida huhudumu kwa kipindi cha miaka minne.

    George, afisa wa kijeshi ambaye alihitimu kutoka chuo cha kijeshi cha West Point, aliteuliwa kwa jukumu hilo mnamo 2023 na Rais wa zamani Joe Biden.

    Mabadiliko ya hivi punde yanakuja baada ya Trump kusema katika hotuba yake kwa taifa kwamba vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vinatarajiwa kumalizika "hivi karibuni".

    George aliwahi kuwa afisa wa jeshi katika Vita vya kwanza vya Ghuba na katika migogoro ya hivi majuzi nchini Iraq na Afghanistan.

    Haijabainika kwa nini alitakiwa kuondoka. "Tunashukuru kwa utumishi wake, lakini ulikuwa wakati wa mabadiliko ya uongozi katika Jeshi," afisa mkuu wa ulinzi ambaye hakutajwa jina aliiambia CBS.

    Msemaji wa Pentagon Parnell alisema: "Idara ya Vita inashukuru kwa miongo kadhaa ya utumishi wa Jenerali George kwa taifa letu. Tunamtakia kila la heri anapostaafu."

    Nafasi yake itachukuliwa na Makamu Mkuu wa Jeshi Jenerali Christopher LaNeve ambaye atakuwa kaimu mkuu wa majeshi, kulingana na vyombo vya habari vya Marekani.

    Soma pia:

  20. Kushambulia miundo mbinu ya raia hakutaifanya Iran kusalimu amri - Araghchi

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema kulengwa kwa daraja la B1 kwenye barabara kuu ya Tehran-Kaskazini hakutaifanya nchi hiyo kusalimu amri.

    Bwana Araghchi aliandika kwenye Mtandao wa X: "Kulenga miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na madaraja ambayo ujenzi wake bado unaendelea, kamwe hakutawashinikiza Wairani kusalimu amri... Kila daraja na kila jengo litajengwa upya kwa ustadi zaidi; lakini jambo ambalo kamwe halitarekebishwa ni uharibifu unaofanywa kwa na Marekani."

    Saa kadhaa zilizopita, Donald Trump alichapisha video ya shambulio la Marekani dhidi ya daraja hilo kwenye mtandao wake wa kijamii, akiandika: "Ni wakati wa Iran kufikia makubaliano kabla ya muda kuwapa kisogo na kuiacha nchi ikiwa imesambaratika."

    Maelezo zaidi:

Trending Now