Mtoto wa kwanza nchini Uingereza kuzaliwa kwa kutumia tumbo la uzazi lililopandikizwa

Chanzo cha picha, PA Media
Mtoto wa kiume amekuwa mtoto wa kwanza nchini Uingereza kuzaliwa kwa kutumia tumbo ya uzazi lilopandikizwa kutoka kwa mtu aliyefariki.
Grace Bell, ambaye ana umri wa miaka 30 na alizaliwa bila tumbo la uzazi, anasema mwanae Hugo ambaye sasa ana wiki kumi tangu kuzaliwa "Ni muujiza."
Bell na mpenzi wake Steve Powell, kutoka eneo la Kent, walimshukuru aliyewapa tumbo la uzazi pamoja na familia yake kwa "ukarimu wao na kujitolea kwao kuwapa zawadi muhimu". Pia waliwashukuru timu ya madaktari kutoka Oxford na London ambao waliwasaidia katika safari yao ya kupata mtoto.
Madaktari wa upasuaji waliohusika na uzalishaji huo walisema "ilikuwa tukio la kihistoria" la kuwapa matumaini wanawake wengine wenye matatizo ya tumbo la uzazi.
"Zawadi muhimu"
Hugo alizaliwa kabla ya sikukuu ya Krisimasi 2025, akiwa na uzani wa takriban kilo tatu katika hospitali ya Queen Charlotte's na Chelsea magharibi mwa London.
Bell ni miongoni mwa wanawake 5000 nchini Uingereza ambao wameathirika na ugonjwa wa MRKH syndrome, kumaanisha alizaliwa bila tumbo la uzazi, huwa hapati hedhi, ila ana mayai ya uzazi.
Akiwa umri wa miaka 16, aliambiwa kuwa hawezi kubeba mimba mwenyewe.
Ili kupata mtoto, yeye na mpenzi wake waliamua kufanya upasuaji wa kupandikiza tumbo la uzazi au kutafuta mtu atakaye wabebea mimba.
Walipopigiwa simu kuwa kuna mtu amewapa msaada wa tumbo la uzazi na kuwa upasuaji wa kupandikizwa tumbo hilo unaweza kufanyika, Bell anasema "nilipigwa na butwaa na nilikuwa na furaha."
Bell anaongezea alikuwa anafahamu jinsi "zawadi hii ni muhimu" na ingemwezesha kubeba mimba na kujifungua mtoto wake mwenyewe.
"Mimi huwaza kila siku kuhusu aliyenipa tumbo la uzazi na familia yake, nawaombea kila siku, kuwa wapate amani ya kujua mtoto wao alinipa zawadi kubwa sana" Alisema Bell.

Chanzo cha picha, PA Media
Upasuaji wa kumpadikiza Bell tumbo la uzazi, ulichukua saa 10 katika hospitali ya The Churchill Hospital eneo la Oxford mwezi Juni 2024.
Miezi kadhaa baadaye, alianza matibabu ya IVF, ikafuatiwa na kuwekewa kiinitete katika hospitali ya The Lister Fertility Clinic mjini London.
Hugo alipozaliwa, Bell alisema "ni muujiza"
"Nakumbuka nikiamka asubuhi na kuona uso wake mdogo, ilihisi nikama ni ndoto"

Chanzo cha picha, Womb Transplant UK/PA Wire
Upandikizaji wa tumbo la uzazi wa Bell kutoka kwa mtu aliyefariki ni moja kati ya upandikizaji 10 wa aina hii unaofanyiwa utafiti na majaribio ya kitabibu nchini Uingereza. Upandikizaji wa tatu tayari umefanywa, ila huyu ndiyo mtoto wa kwanza kuzaliwa.
Mapema mwaka wa 2025, mtoto kwa jina Amy, alizaliwa katika upandikizaji wa kwanza wa tumbo la uzazi nchini Uingereza, baada ya mama ya mtoto huyo kupewa tumbo la uzazi na dadake mwaka wa 2023. Dadake tayari alikuwa na watoto wawili.
Upasuaji zingine tano za kupandikiza tumbo la uzazi kutoka kwa jamaa wa karibu nchini Uingereza zimeratibiwa kufanyika.
Matumani kwa wanawake waliozaliwa bila tumbo la uzazi
Amy alizaliwa katika hospitali moja alikozaliwa Hugo.
Daktari wa uzazi Prof Richard Smith, kutoka imperial College Healthcare NHS Trust, alianza kufanya utafiti kuhusu kupandikiza tumbo la uzazi miaka 25 iliyopita na alikuwepo wakati Hugo alikuwa anazaliwa.
Alisema kuwa "timu wa watu wengi" ilihusika katika mchakato huo, kuanzia kupandikiza, kuwekewa kiinitete hadi kujifungua.
Bell na Powel walimshukuru Smith na kumpa mtoto wao jina Richard, ambaye pia ameanzisha wakfu wa charity Womb Transplant UK.
Wapenzi hao wawili pia wamesema wako tayari kupata mtoto wa pili,kisha madaktari watatakiwa kuondoa tumbo hilo la uzazi. Hii ni kumzuia Bell kutochukua madawa mengi maisha yake yote ambayo yanaweza kuathiri kinga yake ya mwili au kiungo kingine cha mwili.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Daktari wa upasuaji aliyeongoza wataalam waliofanya upandikizi huo Isabel Quiroga , alisema "amefurahishwa" na kuzaliwa kwa Hugo kwani ni historia katika sekta upandikizaji nchini Uingereza.
"Ni watoto wachache sana wamezaliwa Ulaya baada ya mama zao kupandikizwa tumbo la uzazi kutoka kwa mtu aliyefariki." Alisema.
"Tunajaribu kuona iwapo utafiti wetu utafanya utaratibu huu kutumika kama matibabu ya kawaida kwa wanawake ambao hawawezi kubeba mimba"
Smith anasema kujifungua huku kumeonyesha kuwa wanawake wenye umri mdogo ambao waliambiwa hawawezi kujifungua sasa wanamatumanini ya kupata mimba na kuzaa.
Mtoto anayezaliwa kupitia tumbo la uzazi lililopandikizwa hana uhusiano wowote wa kinasaba na aliyetoa ufadhili wa tumbo hilo.
Zaidi ya upasuaji 100 za kupandikiza tumbo la uzazi, zimefanyika kote duniani, na zaidi ya watoto 70 wamezaliwa kutoka mchakato huo.
Kutoa ufadhili wa tumbo la uzazi si kama kutoa viungo vingine vya mwili kama moyo na figo. Lazima mtu anayetaka tumbo la uzazi, kuomba familia inayoweza kumfadhili au kumwomba mtu ambaye yuko tayari kutoa vioungo vyake vya mwili.
Nchini Uingereza, labda ukatae mwenyewe kutoa viuno vyako vya mwili, ila ukifariki viungo vyako vinaweza kuchukuliwa.
Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula











