Theia: Sayari inayotajwa kugongana na dunia na kuunda Mwezi

j

Chanzo cha picha, Getty Images/Mark Garlick

Muda wa kusoma: Dakika 6

Wakati mwingine utakapoutazama mwezi mpevu, fikiria kuhusu Theia.

Hilo ndilo jina ambalo wanasayansi wametoa kwa sayari ya kufikirika ambayo huenda iligongana na Dunia changa takribani miaka bilioni 4.5 iliyopita, na kutoa kipande cha mabaki kilichokuja kuwa Mwezi wetu.

Mgongano mkubwa angani

Wanasayansi kwa sasa wanaamini kwamba mgongano mkubwa kati ya dunia ya mwanzo na kitu kilichokuwa na ukubwa wa Mars ulitoa mabaki ya kutosha ambayo baadaye yaliungana na kuunda Mwezi.

Nadharia hii inajulikana kama Giant Impact Hypothesis. Tukio hilo pia lilianzisha uhusiano ambao umuhimu wake kwa maisha kama tunavyoyajua hauwezi kupingika.

Miongoni mwa mambo mengine, mwezi huweka nguvu ya uvutano na sayari yetu Dunia ambao kwa mabilioni ya miaka umeisaidia kuendelea kuwa thabiti inapozunguka kwenye mhimili wake, jambo lililochangia uthabiti wa hali ya hewa.

"Bila uthabiti wa hali ya hewa, tungekuwa na hali mbaya zaidi za hewa na mabadiliko makubwa ya tabianchi, ambazo hazingekuwa nzuri kwa maendeleo ya uhai," anaeleza Thorsten Kleine, mwanasayansi wa sayari katika taasisi ya Max Planck for Solar System Research nchini Ujerumani.

Kleine alikuwa sehemu ya timu ya kimataifa ya watafiti ambao Novemba mwaka jana walijaribu kutoa mwanga zaidi kuhusu tukio hilo kubwa na la siri la kukutana kwa Dunia na kitu kingine angani.

Katika makala iliyochapishwa katika jarida la kisayansi, Science, timu hiyo ilichambua muundo wa kemikali wa sampuli kutoka katika Dunia na Mwezi, na kuthibitisha nadharia kwamba Theia na sayari yetu zilikuwa kama majirani waliogongana kwa bahati mbaya katika kipindi cha vurugu wakati wa kuundwa kwa Mfumo wa Jua.

Misheni za Apollo za miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970 zilikuwa muhimu kwa uelewa wetu wa Mwezi, ikiwa ni pamoja na jinsi ulivyoweza kuumbwa.

Chanzo cha picha, POT

Maelezo ya picha, Misheni za Apollo za miaka ya 1960 na mwanzoni mwa miaka ya 1970 zilikuwa muhimu kwa uelewa wetu wa Mwezi, ikiwa ni pamoja na jinsi ulivyoweza kuumbwa.

Mwezi mmoja, Nadharia nyingi

Lakini hatukuwa tukiizingatia kila mara Theia.

Kabla wanadamu hawajafika juu ya uso wa Mwezi mwaka 1969, kulikuwa na nadharia kuu tatu nyingine kuhusu asili ya Mwezi.

Kwa mujibu wa nadharia ya Fission, Mwezi uliundwa wakati Dunia ya mwanzo ilipozunguka kwa kasi sana na kutupa kipande cha nyenzo yake kwenda angani.

Nadharia ya Capture ilisema kwamba Mwezi uliundwa sehemu nyingine katika mfumo wa jua na baadaye ukavutiwa na nguvu ya uvutano ya Dunia ilipopita karibu nayo.

Mwisho, kulikuwa na Co-formation Theory, ambayo inasema kwamba Dunia na Mwezi viliundwa pamoja na kutulia karibu na kila kimoja tangu mwanzo.

Badala ya kuonesha ni ipi kati ya nadharia hizi ilikuwa sahihi zaidi, iligundulika kwamba misheni za NASA Apollo zilielekeza kwenye nadharia mpya kabisa.

Kufanana kwa kemikali

Ingawa mafanikio ya Neil Armstrong na wanaanga wengine waliotua kwenye Mwezi mara nyingi hutawala simulizi, mafanikio muhimu ya misheni za Apollo yalikuwa pia katika vitu walivyoleta kutoka safari hiyo.

"Wanaanga wa Apollo walirudisha sampuli za miamba ya Mwezi, na zilipochunguzwa, wanasayansi waligundua kwamba miamba hiyo ilikuwa na kufanana sana kwa kemikali na miamba ya Dunia," anasema Raman Prinja, mwanaastronomia wa Chuo Kikuu London na mwandishi wa kitabu cha sayansi cha watoto Wonders of the Moon.

Hili lilionesha kwamba huenda Mwezi ulitokana na Dunia.

Sampuli za mwezi zilizoletwa Duniani na misheni za Apollo bado zinachunguzwa.

Chanzo cha picha, NASA/Getty Images

Maelezo ya picha, Sampuli za mwezi zilizoletwa Duniani na misheni za Apollo bado zinachunguzwa.

Raman Prinja pia anasema kwamba miamba hiyo inaonesha dalili za kuundwa chini ya joto kali sana, jambo linaloashiria kwamba ilitokana na mgongano mkubwa.

Pia inaonekana kwamba miamba hiyo ilipoteza sehemu kubwa ya chembechembe ambazo huyeyuka kwa urahisi zinapopata joto, jambo linaloonesha kwamba Mwezi ulikuwa katika hali ya kuyeyuka ulipoundwa.

Sarah Valencia, mwanajiolojia wa Mwezi katika NASA, anaongeza kuwa dalili zinazotolewa na sampuli hizo ni sehemu ndogo tu ya ushahidi uliopo.

Maendeleo ya teknolojia katika miongo ya hivi karibuni, hasa kutumia kompyuta kuiga hali za awali, yameimarisha nadharia kwamba Mwezi uliundwa kutokana na mgongano mkubwa.

Kuna hata nadharia zinazosema kwamba mwelekeo wa mhimili wa Dunia, ulisababishwa na mgongano na Theia.

Valencia anasema kwamba nadharia ya Mgongano Mkubwa bado ndiyo njia bora ya kueleza muundo wa kemikali na uhusiano uliopo kati ya Dunia na Mwezi.

Je, Dunia ingeweza kuungana kabisa na sayari ya kufikirika Theia

Lakini nini kilitokea kwa Theia?

Hili ni moja ya mafumbo yaliyobaki.

Tofauti na asteroid maarufu ambayo iligonga Dunia miaka milioni 65 iliyopita, ikiuua dinosaria na kuacha kizaazaa kikubwa kwenye Peninsula ya Yucatan nchini Mexico, Theia haionekani kuacha alama yoyote inayoonekana.

Kwa nini? Kleine anadai kuwa Theia ilikuwa na takriban 10% ya ukubwa wa Dunia, na tofauti hiyo inamaanisha kwamba ingegawanyika wakati wa mgongano na kuingizwa kwa kiasi kikubwa na sayari yetu.

Vipande vyake pia vinaweza kuwa sehemu ya mchanganyiko uliotoa mwanzoni Mwezi.

"Hili lingekuwa matokeo ya asili ya mgongano kama huo. Lakini tungeweza kutarajia kuona alama za muundo wa kemikali wa Theia kwenye Mwezi, jambo ambalo hatujaliona hadi sasa," anasema mwanasayansi huyo.

Wanasayansi wanashuku kwamba Theia na Dunia vilikuwa na muundo wa msingi sawa, kama vile Zuhura (kushoto) na Dunia (kulia) zenye sifa zinazofanana.

Chanzo cha picha, NASA/JPL-Caltech/ESA

Maelezo ya picha, Wanasayansi wanashuku kwamba Theia na Dunia vilikuwa na muundo wa msingi sawa, kama vile Zuhura (kushoto) na Dunia (kulia) zenye sifa zinazofanana.

"Ufafanuzi mmoja ni kwamba Dunia na Theia zilikuwa sawa sana kwa sababu ziliundwa katika eneo moja la mfumo wa jua," anaongeza, na kwa hivyo zilikuwa ngumu kutofautisha.

Vivyo hivyo, tunajua kuwa sayari yetu ina sifa nyingi zinazoshirikiana na majirani wake wawili wa karibu, Venus na Mars.

Venus mara nyingine huitwa "dada mwovu wa Dunia."

"Lakini, kama asili ya Theia haijulikani kwa hakika, vivyo hivyo hatujui hatima yake," anatoa onyo Valencia.

Hata hivyo, kuna baadhi ya dalili.

Utafiti wa mwaka 2023 ulibaini kwamba maeneo mawili makubwa yenye ukubwa wa mabara, yaliyo ndani kabisa ya Dunia, ni mabaki ya Theia.

Kurejea kwenye mwezi

Bado kuna mengi ya kujifunza kuhusu jinsi Dunia na Mwezi zilivyokuwa sambamba, ndiyo sababu wanasayansi wanavutiwa sana na misheni ya sasa ya NASA Artemis na kurudi kwa wanadamu kwenye Mwezi.

Bado kuna maswali mengi kuhusu Mwezi, kwa hivyo NASA inapanga kuwatuma wanadamu kwenye uso wake tena katika miaka ijayo.

Chanzo cha picha, NASA

Maelezo ya picha, Bado kuna maswali mengi kuhusu Mwezi, kwa hivyo NASA inapanga kuwatuma wanadamu kwenye uso wake tena katika miaka ijayo.

Mbali na majaribio ya hali ya juu zaidi kuliko yale yanayowezekana katika enzi ya Apollo, misheni za hivi karibuni zitachunguza maeneo mapya ya Mwezi, kama vile Ncha yake ya Kusini.

Sampuli za mwezi zilizoletwa Duniani na Apollo zinatoka katika eneo dogo la Mwezi: eneo la ikweta la uso unaoonekana.

"Kama tungetembelea maeneo sita tu Duniani, je, tungeweza kusema kwamba tumechunguza Dunia nzima na kuelewa? Bila shaka sivyo! Mwezi una uwezo usioisha wa kisayansi," anasema Valencia.

Lakini kwa sasa, kwa yale ambayo tayari tumejifunza, ni sawa kusema tunaweza kuishukuru sana Theia kwa kujitolea kwake.