Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Iran yakanusha madai ya Trump kwamba imeomba kusitishwa kwa mapigano
Tangu Marekani na Israel zilipoanza mashambulizi ya anga dhidi ya Iran mnamo tarehe 28 Februari, viongozi kadhaa wakuu wa Iran wameuawa
Muhtasari
- Iran yakanusha madai ya Trump kwamba imeomba kusitishwa kwa mapigano
- Iran inawatumia watoto katika vita vinavyoendelea - Ripoti
- Uingereza kuwa mwenyeji wa kongamano la kimataifa kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz
- Nani amemwomba Trump asitishe mapigano?
- Marekani huenda ikajiondoa Nato - The Telegraph
- Bunge la Tanzania laitisha kikao cha dharura kujadili ongezeko la bei ya mafuta
- Wapalestina waliopatikana na hatia wakabiliwa na adhabu ya kifo chini ya sheria mpya ya Israel
- Raia wa Iran wanazuiwa kuingia au kupitia UAE - Shirika la ndege la Emirates
- Watu 29 wafariki katika ajali ya ndege ya jeshi la Urusi huko Crimea
- Ethiopia yawakamata watu 658 kwa kuhusika na biashara haramu ya mafuta
- Mwanahabari wa Marekani Shelly Kittleson atekwa nyara mjini Baghdad
- Beirut yakumbwa na mashambulizi 'makali' Israel ikiwalenga viongozi wa Hezbollah
- Israel yapinga kuhusika na mlipuko uliowaua walinda amani Umoja wa Mataifa
- Tuanzebe airejesha DR Congo kwenye Kombe la Dunia baada ya miaka 52
- Trump asema Marekani itaondoka Iran ndani ya 'wiki mbili au tatu' iwe 'kuna makubaliano au la
Moja kwa moja
Na Ambia Hirsi & Asha Juma
Iran yakanusha madai ya Trump kwamba imeomba kusitishwa kwa mapigano
Wizara ya mambo ya nje ya Iran imesema madai ya Rais Donald Trump kwamba nchi hiyo imeomba mapigano yasitishwe ni "ya uwongo na hayana msingi".
Televisheni ya taifa ya Iran inaripoti matamshi hayo kama yalivyosemwa na msemaji wa wizara ya mambo ya nje Esmaeil Baqaei.
Hii inakuja baada ya Trump kusema hapo awali, katika ujumbe kwenye mtandao wa Truth Social kwamba "Rais Mpya wa Utawala wa Iran", ambaye hakumtaja jina, alikuwa ameomba kusitisha mapigano - na kwamba anaweza tu kufikiria kuhusu ombi hilo ikiwa "Mlango-Bahari wa Hormuz utafunguliwa, kuachwa huru, na wazi".
Som zaidi:
Iran inawatumia watoto katika vita vinavyoendelea - Ripoti
Kifo cha mvulana mmoja nchini Iran mwenye umri wa miaka 11 aliyekuwa na babake, kiliripotiwa baada ya mashambulizi ya anga kulenga kivuko kimoja mjini Tehran ambapo walikuwa wanashika doria.
Mamake Alireza Jafari, aliambia gazeti linalosimamiwa na manispaa ya Hamshahri kuwa wawili hao walikuwa wakiwasaidia polisi wa Basij kushika doria katika maeneo ya ukaguzi ili “kudumisha usalama wa Tehran na wakazi wake.”
Wawili hao waliuawa tarehe 11 mwezi Machi.
Wiki iliyopita, afisa mmoja wa Jeshi la Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) mjini Tehran aliliambia shirika la habari la Fars kuwa IRGC inapania kuwasajili “wanajeshi wakujitolea” wenye umri wa kuanzia miaka 12 na kuendelea.
Baadhi ya wakazi wameiambia BBC kwamba wamewaona watoto, wengine wakiwa na silaha, wakishika doria katika maeneo ya ukaguzi katika mji mkuu wa Tehran na maeneo mengine.
Mashirika ya haki za binadamu pia yameripoti kifo cha Alireza. Kundi la Wakurdi la Hengaw limesema alikuwa “mwanafunzi wa darasa la tano aliyeuawa akiwa kwenye kituo cha ukaguzi mjini Tehran."
Mama yake Alireza alisema kuwa mumewe alimwambia kuwa hakukuwa na polisi wa kutosha kwenye kituo hicho, na “walikuwa watu wanne tu” waliokuwepo. Alisema mumewe alimchukua Alireza na kumwambia mtoto huyo kuwa anahitaji kuwa “tayari kwa siku zijazo.”
Alisema mwanawe alimwambia “mama, tutashinda vita hivi au tutakuwa wafia dini. Ikiwa Mungu atakubali, tutashinda, lakini ningependa kuwa mfia dini.”
Gazeti la Hamshahri nchini Iran limesema wawili hao waliuawa na “shambulio la droni la Israel.”
Pia unaweza kusoma :
Uingereza kuwa mwenyeji wa kongamano la kimataifa kuhusu Mlango Bahari wa Hormuz
Waziri mkuu wa Uingereza Keir Starmer ametangaza kuwa taifa lake litakuwa mwenyeji wa kongamano la viongozi wa kimataifa kujadili jinsi ya kufungua Mlango Bahari wa Hormuz na kurejesha uhuru wa usafiri katika eneo hilo la bahari.
Usafiri kupitia mlango huo wa bahari umeathirika kufuatia hatua za Iran kuzuia meli kupita eneo hilo baada ya kushambuliwa na Marekani na Israel. Hali hii imesababisha kupanda kwa bei ya mafuta duniani.
Starmer pia amerejelea tena kauli yake ya awali kwamba Uingereza haitajihusisha na mzozo wa Mashariki ya Kati, na kwamba njia bora ya kukabiliana na kupanda kwa gharama ya maisha ni kushinikiza vita hivyo kumalizika na kuhakikisha Mlango Bahari wa Hormuz unafunguliwa tena.
Pia unaweza kusoma:
Nani amemwomba Trump asitishe mapigano?
Iran imekanusha madai ya Trump kwamba inahusika katika mazungumzo ya kukomesha vita, ikisema ni baadhi tu ya jumbe zimebadilishwa na Marekani kupitia wapatanishi.
Trump alisema "Rais Mpya wa Utawala wa Iran" amemwomba asitishe mapigano.
Haijulikani wazi anamzungumzia nani.
Tangu Marekani na Israel zilipoanza mashambulizi ya anga dhidi ya Iran mnamo tarehe 28 Februari, viongozi kadhaa wakuu wa Iran wameuawa, akiwemo Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei
Alirithiwa na mwanawe, Mojtaba Khamenei, mnamo Machi 8. Ametoa taarifa kadhaa zilizoandikwa tangu wakati huo lakini hajawahi kuonekana hadharani. Trump mwenyewe amesema hajui kama yuko hai.
Iran haina rais mpya. Masoud Pezeshkian, aliyechaguliwa mwaka wa 2024, amejitokeza hadharani – hapo jana, kulingana na vyombo vya habari vya Iran. Alisema jana kwamba Iran ilikuwa na "nia muhimu" ya kukomesha vita.
Soma zaidi:
Habari za hivi punde, Trump asema Iran imeomba kusitisha mapigano
Donald Trump anasema "Rais Mpya wa Utawala wa Iran" ameiomba Marekani kusitisha mapigano.
Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Truth Social, hamtaji afisa huyo mkuu kwa jina, lakini anaeleza kwamba mtu huyo "hana msimamo mkali sana na mwenye akili zaidi kuliko watangulizi wake".
Ameongeza: "Tutazingatia hilo wakati Mlango-Bahari wa Hormuz utakapofunguliwa, kuwa huru, na wazi. Hadi wakati huo, tunaiangamiza Iran au, kama wanavyosema, kurudi kwenye Enzi za Kutumia Vifaa vya Mawe!!!"
Soma zaidi:
Trump asema anafikiria kuondoka Nato
Rais wa Marekani Donald Trump amesema “anafikiria” kuiondoa Marekani kutoka kwa muungano wa kujihami wa Nato, hii ni kulingana na mahojiano aliyofanya na gazeti la The Telegraph
Kulingana na gazeti hilo, Trump alisema Nato “haina nguvu” akiikosoa Uingereza kwa kukosa jeshi la wanamaji.
Trump alisema anazingatia kuunda muungano na mataifa ya Mashariki ya Kati baada ya vita kumalizika.
“Sijawahi kushawishika na Nato, nilijua hawana nguvu, hata Putin anajua hilo pia,” alisema Trump.
“Hawana hata jeshi la wanamaji. Wana ndege za kivita zilizozeeka na hazifanyi kazi,” Trump alisema akiikashifu Uingereza.
Pia unaweza kusoma:
Bunge la Tanzania laitisha kikao cha dharura kujadili ongezeko la bei ya mafuta
Spika wa Bunge nchini Tanzania, Mussa Zungu amemuagiza Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi kukutana na Kamati ya Bunge ya Nishati ili kujua hatma ya hali na mwenendo wa kupanda kwa bei ya mafuta nchini Tanzania.
“Bila mafuta tunaweza kukwama kwenye mipango ya nchi na mambo mengine ya maendeleo”alisema Zungu.
Hayo yanajiri baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kutangaza bei elekezi mpya za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa zilizoanza kutumika rasmi leo Aprili Mosi, 2026, ikiwa ni sehemu ya marekebisho ya kila mwezi yanayozingatia mwenendo wa soko la dunia.
Zungu amesisitiza kwamba serikali itatoa taarifa yake kuhusu mwenendo wa mafuta baada ya kamati kukutana na kujadili.
Kulingana na Mamlaka ya Udhibiti ya Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania EWURA, kupanda kwa bei hizo kumetokana na ongezeko kubwa linalosababishwa na mzozo unaoendelea Mashariki ya kati dhidi ya Iran.
Bei ya lita ya petroli jijini Dar Es Salaam imepanda kwa shilingi 956 za Tanzania ambayo ni sawa na dola senti 37 na kuzua hisia kali miongoni mwa raia wa taifa hilo.
Kwa mujibu wa bei mpya mjini Dar es Salaam Petroli sasa itauzwa kwa shilingi za Tanzania 3,820, Dizeli Sh 3,806, Mafuta ya Taa Sh 3,684.
Kulingana na Ewura mashambulizi katika visima vya mafuta, maghala na viwanda vya kusafisha mafuta katika eneo la mashariki ya kati pamoja na kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz unaopitisha takriban asilimia 20 ya mafuta yote duniani ndio sababu inayochangia kupanga kwa gharama ya uagizaji wa bidhaa hiyo nchini Tanzania.
Soma zaidi:
Wapalestina waliopatikana na hatia wakabiliwa na adhabu ya kifo chini ya sheria mpya ya Israel
Bunge la Israel limeidhinisha sheria ambayo itafanya adhabu ya kifo kuwa isiopingika kwa Wapalestina waliopatikana na hatia ya mashambulizi ya kigaidi.
Wakosoaji, akiwemo mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk, wameelezea sheria hiyo mpya kama ya kibaguzi. Türk pia ilisema matumizi yake "yatakuwa uhalifu wa kivita".
Sheria mpya ilipitisha usomaji wake wa tatu na wa mwisho katika bunge la Knesset kwa kura 62 dhidi ya 48 Jumatatu, huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akipiga kura ya kuunga mkono.
Muswada huo unaeleza kwamba Wapalestina waliopatikana na hatia katika mahakama za kijeshi za Israeli kwa kufanya mashambulizi hatari yanayodhaniwa kuwa "vitendo vya ugaidi" watauawa kwa kunyongwa ndani ya siku 90, huku kukiwa na uwezekano wa kuahirishwa kwa hadi siku 180.
Kinadharia, Wayahudi wa Israeli wataweza pia kunyongwa chini ya sheria - lakini kiutendaji wa hili haukaribii kutokea, kwani adhabu ya kifo inaweza tu kutekelezwa pale ambapo nia ya shambulizi hilo ilikuwa "kupinga uwepo wa taifa la Israeli".
Sheria hiyo ilishinikizwa vikali na wafuasi wa mrengo wa kulia, huku Waziri wa Usalama wa Taifa Itamar Ben-Gvir akiwa katika mstari wa mbele. Baada ya kura, aliandika kwenye mtandao wa X: "Tumeandika historia!!! Tuliahidi. Tumetekeleza."
Mwanachama wa chama cha Ben-Gvir, Limor Son-Har-Melech, ambaye alinusurika shambulizi la watu wenye bunduki wa Kipalestina ambapo mumewe aliuawa, alisema kwamba sheria hiyo ilikuwa muhimu, akitoa mfano wa jinsi mmoja wa wauaji wa mumewe alivyoachiliwa baadaye na kuendelea kushiriki katika mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israel.
Wakati wa mjadala katika bunge la Knesset, alisema: "Kwa miaka mingi, tumevumilia mzunguko mkali wa ugaidi, kifungo, kuachiliwa huru katika mikataba ya kiholela, na kurudi kwa viumbe hawa wabaya wa kibinadamu kuwaua Wayahudi tena."
Soma zaidi:
Raia wa Iran wanazuiwa kuingia au kupitia UAE - Shirika la ndege la Emirates
Tovuti ya shirika la ndege la Emirates lenye makao yake Dubai ilisema Jumatano kwamba raia wa Iran hawaruhusiwi kuingia au kusafirisha katika nchi ya Falme za Kiarabu.
Tovuti ya shirika lingine la ndege, Flydubai, ilisema raia wa Iran walio na "Golden Visa" ya UAE wameondolewa kwenye kundi hilo na wanaruhusiwa kuingia na kuunganisha safari zao kupitia nchini hiyo.
Vizuizi hivyo vinakuja huku kukiwa na mvutano ulioongezeka kati ya Iran na mataifa ya Ghuba.
Soma zaidi:
Watu 29 wafariki katika ajali ya ndege ya jeshi la Urusi huko Crimea
Ndege ya kijeshi ya Urusi imeanguka huko Crimea na kusababisha vifo vya watu 29, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imeambia vyombo vya habari vya serikali.
Mabaki ya ndege hiyo aina ya An-26 yalipatikana baada ya ndege hiyo kupoteza mawasiliano na mamlaka wakati wa "safari ya kawaida", wizara iliambia mashirika ya habari ya Urusi Tass na Ria-Novosti.
Masuala ya kiufundi yanaonekana kusababisha ndege hiyo kuanguka kwenye mwamba, ikiwa na wafanyakazi sita na abiria 23, wizara ilinukuliwa ikisema. Haionekani kuwa na waathirika wowote. Urusi iliteka rasi ya Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014.
Wizara hiyo iliripoti kuwa hakuna uharibifu wowote wa nje wa ndege hiyo, ikimaanisha kwamba makombora, ndege zisizo na rubani au ndege hazishukiwa kusababisha ajali hiyo.
Tass iliripoti kuwa mawasiliano na ndege hiyo yalipotea takriban saa 18:00 kwa saa za ndani (15:00 GMT) siku ya Jumanne, na mabaki hayo yalipatikana kufuatia juhudi za utafutaji na uokoaji.
Ndege ya An-26 ni ndege ya enzi za Usovieti inayotumika hasa katika uwezo wa kijeshi kusafirisha mizigo mizito na idadi ndogo ya abiria.
Inatengenezwa na kampuni ya anga ya Ukrainei ya Antonov.
Ndege hizo zimetumika tangu mwishoni mwa miaka ya 1960, lakini zimehusika katika ajali kadhaa mbaya.
Pia unaweza kusoma:
Ethiopia yawakamata watu 658 kwa kuhusika na biashara haramu ya mafuta
Watu 658 wamekamatwa nchini Ethiopia, wakiwemo maafisa wa serikali, wanaoshukiwa kujihusisha na biashara haramu ya mafuta na kuhodhi bidhaa hiyo muhimu wakati nchi inakabiliwa na uhaba kutokana na vita vya Iran, gazeti la kibinafsi la Addis Standard linaripoti.
Waziri wa Biashara Kasahun Gofe alisema kuwa kukamatwa kwa watu hao ni sehemu ya hatua za kiutendaji zilizoimarishwa chini ya kikosi kazi kipya kilichopewa jukumu la kufuatilia usambazaji wa mafuta kote nchini.
Kasahun alionya kuwa usambazaji wowote wa mafuta nje ya mfumo uliowekwa utachukuliwa kuwa kinyume cha sheria na yeyote atakayepatikana na hatia atakabili na adhabu kali, huku mamlaka ikiendelea na juhudi za kudhibiti biashara haramu ili kuleta utulivu wa soko.
Wakati huo huo, waziri huyo alisema kuwa wasambazaji wa mafuta katika eneo la Mashariki ya Kati wameshindwa kuwasilisha tani 180,000 za mafuta nchini Ethiopia wakati wa vita.
Kulingana na ripoti hiyo, mamlaka ilikuwa imenasa zaidi ya lita 720,000 za mafuta, na kuirejesha katika udhibiti wa serikali wakati vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran huku usambazaji wa dizeli ya kila siku ya Ethiopia ikipunguzwa kutoka lita milioni 9.2 hadi milioni 4.5.
Maelezo zaidi:
Mwanahabari wa Marekani Shelly Kittleson atekwa nyara mjini Baghdad
Mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Marekani ametekwa nyara katika mji mkuu wa Iraq Baghdad, na mmoja wa washukiwa anahusishwa na wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran, maafisa wa Iraq na Marekani wanasema.
Shelly Kittleson alitekwa nyara siku ya Jumanne jioni, ilisema Al-Monitor, chombo cha habari ambacho amechangia makala zake.
Wizara ya mambo ya ndani ya Iraq imesema kuwa vikosi vya usalama viliwakimbiza watekaji nyara wa mwandishi huyo katika msako uliosababisha gari moja la watekaji hao kupinduka na kukamatwa kwa mshukiwa mmoja.
Afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani alisema mtu mmoja aliyekuwa na uhusiano na kundi la wanamgambo wenye mafungamano na Iran, Kataib Hezbollah, alizuiliwa na mamlaka ya Iraq.
Dylan Johnson, waziri msaidizi wa mambo ya nje wa masuala ya umma duniani, alithibitisha kutekwa nyara kwa mwandishi wa habari wa Marekani, bila kumtaja Kittleson.
Alichapisha kwenye mtandao wa X: "Idara ya Jimbo hapo awali ilitimiza jukumu letu la kuonya mtu huyu kuhusu vitisho dhidi yao na tutaendelea kuratibu na FBI ili kuhakikisha kuachiliwa kwao haraka iwezekanavyo."
Inafahamika kuwa maafisa wa Marekani walikuwa wamewasiliana na Kittleson mara kadhaa kuonya kuhusu vitisho dhidi yake, ikiwa ni pamoja na Jumatatu usiku.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema katika taarifa kwa BBC: "Kutokana na faragha na masuala mengine, hatuna la zaidi la kusema kwa sasa."
Al-Monitor, yenye makao yake nchini Marekani, ilisema ripoti za habari za ndani zinaonyesha kuwa Kittleson alichukuliwa karibu na hoteli katikati mwa mji mkuu.
Iliongeza kuwa idara ya serikali imethibitisha "ina habari kuhusu utekaji nyara wa Kittleson na inashirikiana na serikali ya Iraq kusaidia kuachiliwa kwake".
Beirut yakumbwa na mashambulizi 'makali' huku IDF ikiwalenga viongozi wa Hezbollah
Ripoti zinaonyesha kuwa mji mkuu wa Lebanon, Beirut ulikumbwa na mashambulizi makali ya anga usiku kucha, ambapo jeshi la Israel linasema lilimpiga kamanda wa Hezbollah na kiongozi mwingine mkuu.
IDF inasema ilifanya "mashambulizi mawili tofauti" kote Beirut lakini haikutoa maelezo zaidi.
Moshi ulionekana kupanda kutoka kitongoji cha Jnah nje kidogo ya kusini mwa Beirut, wakati milipuko "mizito" ilitikisa sehemu za jiji, kulingana na maafisa wa usalama wakizungumza na Reuters.
Gari lililokuwa likisafiri kusini mwa Beirut lilishambuliwa kwa makombora mengi yaliyorushwa na ndege isiyo na rubani ya Israel, vyombo vya habari vya serikali ya Lebanon viliripoti.
Mapema siku ya Jumanne, Wizara ya Afya ya Lebanon ilisema watu wanane wameuawa na migomo ya Israel kusini mwa nchi hiyo, akiwemo mhudumu wa afya.
Israel yapinga kuhusika na mlipuko uliowaua walinda amani Umoja wa Mataifa
Israel inasema haikuhusika na mashambulizi yaliyosababisha vifo vya walinda amani wawili wa Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon siku ya Jumatatu.
Matokeo ya awali ya uchunguzi wa Kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (Unifil) yanaonyesha kuwa "mlipuko wa barabarani" ulipiga msafara karibu na Bani Haiyyan, na kuwaua walinda amani wawili wa Indonesia na kujeruhi wengine wawili.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) linasema tukio hili "halikusababishwa na shughuli za IDF".
"Uchunguzi wa kina unaonyesha kwamba hakuna kifaa cha kulipuka kilichowekwa katika eneo hilo na wanajeshi wa IDF, na kwamba hakuna askari wa IDF waliokuwepo katika eneo hilo hata kidogo," inasema katika taarifa.
Inaongeza kuwa inalenga maeneo ya Hezbollah katika eneo hilo, sio Unifil, na iliitaka Unifil "kuepuka kuwepo katika maeneo ya mapigano" ambayo IDF imetoa maagizo kwa watu kuhama.
Soma pia:
Tuanzebe airejesha DR Congo kwenye Kombe la Dunia baada ya miaka 52
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imejihakikishia tiketi ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 52, baada ya Axel Tuanzebe kufunga bao la dakika za nyongeza lililowapa ushindi wa 1-0 dhidi ya Jamaica katika fainali ya mchujo ya bara, iliyopigwa kwenye Uwanja wa Guadalajara nchini Mexico.
Wakati wa maandalizi ya mechi hiyo, Tuanzebe aliliambia BBC kuwa mchezo huo ulikuwa mkubwa zaidi katika maisha yake ya soka.
Beki huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, ambaye alizaliwa Bunia, mji uliokumbwa na machafuko ya muda mrefu mashariki mwa DR Congo, sasa ameandika historia mpya kwa taifa hilo.
Licha ya mshambuliaji wa Leopards, Cédric Bakambu, kukosa mabao mawili yaliyokataliwa kwa kuotea katika muda wa kawaida, haikushangaza kwamba pambano hilo lililokuwa na ushindani mkubwa lililazimika kuamuliwa katika dakika 30 za nyongeza.
Ndipo Tuanzebe alipokuwa mahali sahihi kwa wakati sahihi, akitumia mwili wake kuunganisha mpira wa kona uliopigwa na Brian Cipenga na kuutumbukiza wavuni.
Shangwe zilisitishwa kwa muda huku waamuzi wakipitia tukio hilo kwa VAR kufuatia tuhuma za mpira wa mkono, lakini hatimaye ilithibitishwa kuwa hakukuwa na kosa, na bao hilo likasalia halali.
Kwa upande mwingine, Jamaica waliokuwa wakisaka kufuzu kwa Kombe la Dunia kwa mara ya pili tangu waliposhiriki mwaka 1998 nchini Ufaransa walishindwa kuunda nafasi za maana za kusawazisha bao na badala yake, ni DR Congo ambao sasa watajiunga na Kundi K katika michuano hiyo iliyopanuliwa ya timu 48.
DR Congo wataanza dhidi ya Ureno mjini Houston tarehe 17 Juni, kabla ya kukutana na Colombia na Uzbekistan.
Maelezo zaidi:
Trump asema Marekani itaondoka Iran ndani ya 'wiki mbili au tatu' iwe 'kuna makubaliano au la
Rais Donald Trump amewaambia waandishi wa habari kwamba Marekani "itaondoka[Iran] hivi karibuni" na hatua za kijeshi za nchi hiyo zitakomeshwa ndani ya "wiki mbili au tatu"
Anasema Marekani imefikia malengo iliyojiwekea kabla ya kuanza kwa mashambulizi ya anga dhidi ya Iran mwezi uliyopita kwa ushirikiano na Israel.
Ameongeza kuwa lengo la kuizuia Iran kuwa na uwezo wa kuunda silaha za nyuklia limefikiwa na sasa Marekani "inamaliza kazi"
Trump pia anasema Marekani sasa inatawala anga la Iran na pia imepata mabadiliko ya utawala kufuatia mauaji ya viongozi wakuu wa kisiasa na kijeshi.
Aliwataja viongozi hao wapya mjini Tehran kama "walio na misimamo mikali" na "waadilifu zaidi" ikilinganishwa na watangulizi wao.
Trump pia anasema viongozi wa Iran "wanaomba kufanya makubaliano" na Marekani ili kumaliza vita, madai ambayo hapo awali yalipingwa na Iran.
Anaongeza kuwa vita vinaweza kumalizika bila makubaliano kati ya pande hizo mbili.
Kuhusu athari za vita hasa kupanda kwa bei ya mafuta, rais Trump anasema bei itashuka mara tu Marekani itakapomaliza hatua zake za kijeshi.
Soma zaidi:
Natumai hujambo.